Mafanikio CAF, Simba, Yanga ziwekeze kwa wachezaji bora

Nipashe
Published at 10:58 AM Apr 09 2024
Nembo za klabu ya Yanga na Simba.
PICHA: Maktaba
Nembo za klabu ya Yanga na Simba.

RASMI sasa kuwa Simba na Yanga zitasubiri tena msimu ujao ili kujaribu bahati yao Ligi ya Mabingwa Afrika kama zitaweza tena kufika hatua ya makundi na kuvuka robo fainali baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu huu.

Yanga imeshindwa kuvuka hatua hiyo, kutokana na kuondolewa kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 180 za mechi zote mbili zilizochezwa jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa, na Loftus Versfeld jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Simba imekuwa sasa kama ni kawaida au utamaduni wao kuishia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya msimu huu kuchapwa jumla ya mabao 3-0, ikifungwa nyumbani Benjamin Mkapa, Dar es Salaam bao 1-0 na mabao 2-0, Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, nchini Misri, dhidi ya Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo, Al Ahly.

Ukiangalia jinsi timu za Tanzania zilivyoingia hatua hiyo na zilivyotolewa, si kwamba ni mbaya au zimeshindwa kwenda nusu fainali kwa sababu ya ubovu wa vikosi, au bahati, hapana ni viwango.

Kwanza tunazipongeza klabu hizo na viongozi wao kwa hapo walipofika kwani wameuwakilisha vema Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA na si Tanzania pekee.

Kama nia itakuwa ni kuishia hatua hiyo siku zote sawa, lakini tunaona endapo timu hizo zinataka kusonga mbele zaidi ya hatua hiyo, sasa ziongeze uwekezaji kwa kusajili wachezaji wenye uwezo zaidi ya hawa waliopo.

Michuano ya hii imeonyesha kuwa wachezaji waliopo wanamudu sana kutinga hatua za makundi na pia kupambana na timu zilizopo kwenye makundi, lakini linapokuja suala la robo fainali ndiyo inakuwa mtihani kuvuka hapo.

Sisi tunaona sasa Klabu za Tanzania hususan Simba na Yanga hazina budi kuachana na maneno mengi ya propaganda kutoka kwa maofisa habari wao ambao wamekuwa wakiwaaminisha vitu vingi mashabiki na wanachama wao, ambavyo vingine havipo na ni ndoito kutokea kutokana na ubora wa vikosi vyao na badala yake wawekeze ndani ya uwanja kwa wachezaji bora wenye viwango vya ya hali ya juu ambao watakuwa wanaweza kuamua mechi kubwa za maamuzi kama hizi.

Kwa timu kama ya Yanga ukiitazama haina mapungufu mengi, badala yake inahitaji mshambuliaji katili tu, mithili ya Fiston Mayele mwenye uwezo wa kuamua mechi.

Clement Mzize alikosa bao la wazi ugenini dhidi ya Mamelodi katika mechi ambapo kwa straika wa viwango vya juu, si rahisi kukuacha na kama angefunga mchezo ulikuwa unaishia hapo na kwa mara ya kwanza katika historia Yanga ingetinga nusu fainali ya michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Nayo Simba ikiwa ugenini Cairo ilipiga pasi 521, zaidi ya wenyeji wake ambao walipiga pasi 414 na kuacha wageni wakimiliki mpira kwa asilimia 56 dhidi ya 44 za Al Ahly, wakapiga mashuti 10, wakati wenzao walipiga saba tu.

Pamoja na hayo ni mawili tu yaliyolenga lango, wakati Al Ahly mashuti manne katia ya saba yalilenya lango na kupata mabao mawili. Hii inaonyesha usahihi wa timu zilizowekeza vizuri kutumia nafasi chache zinazopatikana kuzigeuza kuwa mabao kitu ambacho kwa Simba na Yanga ni tatizo.

Hivyo, tunaona kwa Simba mbali ya kutakiwa kusajili straika mawili wa daraja la juu, na si kina Jean Baleke tena na Moses Phiri, bado wanapaswa kusajili mabeki wawili wa pembeni kwani waliopo tunaona wanazidi kushuka ubora wao na hata timu zinazocheza dhidi yao zimeshawasoma kwa sababu miaka nenda rudi ni hao hao tu hawana mbadala.

Tunamini Simba inatakiwa pia kuwa beki mmoja wa kati katili, mwenye nguvu, asiye na mzaha kama alivyokuwa Joash Onyango alipokuwa kwenye kiwango cha juu, kwa sababu imekuwa ikiruhusu mabao kirahisi ambayo kwa timu kubwa kama hiyo hayatakiwi kufungwa.

Aidha, hatutarajii kuziona kila msimu zikisajili wachezaji wapya karibu zaidi ya sita kwani huko nako kunachangia kuunda kikosi cha ushindani kutokana na kuhitaji muda wa kuzoeana.