Serikali inastahili pongezi kupokea kilio cha kikokotoo

Nipashe
Published at 09:02 AM Apr 18 2024
Katuni.
Mchoraji: Abdul Kingo
Katuni.

KUNA msemo kwamba ngoma ikivuma sana mwishowe hupasuka. Pia kuna msemo kwamba mzazi mzuri na bora ni yule amsikilizaye mwanawe kukusu matatizo yanayomkabili na hatimaye kuyapatia ufumbuzi.

Hivyo ndivyo inavyosadifu sasa kuhusu kilio cha miaka kadhaa kuhusu kikokotoo kipya cha mafao ya wastaafu baada ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii kubadilishwa na kanuni mpya ya ukokotoaji mafao ilivyoanza kutumika tangu mwaka 2023. 

Kanuni hiyo mpya inasema bila kujali wafanyakazi hapo ni wa umma au sekta binafsi, kikotoo cha mafao kitakuwa asilimia 33. Baada  ya hapo, mnufaika atapata pensheni kidogo kidogo kwa muda wa miaka 12 na nusu na iwapo atafariki dunia, wategemezi wake watapewa kiasi hicho kwa miaka mitatu kisha kukoma. 

Tangu kuanza kutumika kwa kanuni hiyo, kumekuwa na vilio vingi kutoka kwa watumishi kwamba kiasi wanacholipwa ni kidogo na kinakatisha tamaa. Vyama vya wafanyakazi kupitia shirikisho lao (TUCTA), pia vimekoleza mwangwi wa kilio kuhusu kikokotoo kabla ya kuwafikia wabunge ambao walisimama na kukizungumzia kwa uchungu katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.  

Jambo kubwa lililowafumbua macho ni kuhusu uhalisia wa stahiki ya mtu anayestaafu uliotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo. Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/25, Gambo alisema kwa mtumishi aliyekuwa akipokea mshahara wa Sh. 800,000 kwa kikokotoo  iliyokuwa mifuko ya wafanyakazi serikali za mitaa (LAPF) na watumishi wa umma (PSSF) alikuwa akipata malipo ya mkupuo Sh. 57,466,666 lakini kwa kikokotoo cha sasa anapata Sh. 28,675,862 tofauti ya Sh. milioni 29,190,804.

Mbali na mafao hayo, kila mwezi kustaafu alikuwa anapata Sh. 401,000 kwa kikokotoo cha zamani na cha sasa atapata 388,137. Hali hiyo inaonyesha wazi kwamba kuna uonevu mkubwa kwa wafanyakazi waliotumikia nchi kwa moyo wote kwa zaidi ya miaka 30. 

Baada ya kuibuka upya kwa mijadala mbalimbali ndani na nje ya Bunge kuhusu suala la kanuni mpya ya kikokotoo kipya cha wastaafu, hatimatye serikali imesema imepokea maoni yote yaliyotolewa na wadau pamoja na wabunge na kuahidi kulifanyia kazi.

Kauli hiyo ya serikali liyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kuhitimisha hoja ya makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/25 Jumatatu wiki hii, ni ya kutia faraja na kurejesha matumaini ya wafanyakazi yaliyokuwa yamepotea. Kwa hatua hiyo, serikali imeonyesha ukomavu wake kuwa ni sikivu . 

Bila kuuma maneno, Waziri Mkuu alisema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wastaafu na itaendelea kufanya tathimini kwa kuzingatia sheria za kazi. Pia alisema serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii ikiwamo mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali kuhusu elimu ya mafao. 

Kama alivyosema Waziri Mkuu Majaliwa, wafanyakazi na wadau wana matumaini makubwa kuwa serikali italifanyia kazi jambo hilo ambalo limeshasababisha maumivu kwa baadhi ya watumishi ili wanufaike na jasho walilovijisha kwa zaidi ya miaka 30 ya utumishi wao. Mafao bora kwa mstaafu ni kielelezo cha shukrani kwa utumishi wake uliotukuka ukiambatana na uaminifu kwa muda wote huo. 

Kwa mantiki hiyo, serikali ikutane na wadau kupitia vyama vya wafanyakazi na waajiri ili kuweka sawa suala hilo ambalo halitoi picha nzuri kwa serikali. Jambo la muhimu ni kutambua kwamba mfanyakazi amekaa miaka 30 kwenye ajira, hivyo anatumaini kuwa kustaafu kwake kutampa Faraja na si majuto kama ilivyo kwa kikokotoo kipya. 

Wahenga wanasema penye nia pana njia. Kwa kuwa serikali imetamka kuwa imepokea kilio hicho, ni imani kwamba inayo nia thabiti ya kushughulikia suala hilo na hatimaye wastaafu kuwa na kicheko.