CHADEMA yaitaka serikali kupunguza ugumu wa maisha

By Elizabeth Seleman ,, Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:21 AM Apr 30 2024
Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe.
PICHA: MAKTABA
Mwenyekiti wa chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kufanya maandamano ya amani katika majiji mbalimbali, huku Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiiomba serikali kuangalia kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi.

Ametoa kauli hiyo wilayani Sengerema, mkoani Mwanza wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani.

Mbowe amesema hali ya maisha imekuwa ikipanda kila siku kutokana na baadhi ya vitu muhimu kupanda bei na huku upatikanaji wa fedha kwa wananchi ukiwa mgumu.

Kuhusu Katiba,  amesema ni wakati wa serikali kukaa chini na kufanya maridhiano ili ilete chachu na maendeleo ya taifa, akitaja uhitaji wa Katiba hiyo kuwa ndiyo chanzo kikuu cha kufanya maandamano ya amani.

"Tunafanya maandamo ya amani ili kufikisha hisia zetu pamoja na uchungu wa maendeleo na kuhusu upandaji wa maisha hali ambayo inasababisha ugumu wa maisha kwa watu hasa wenye vipato vidogo,"  amesema Mbowe. 

 Naye Mwenyekiti wa Vijana CHADEMA mkoani Mwanza, Abasi Mayala, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye uboreshaji wa daftari la kupiga kura ili wapate fursa ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Baadhi ya wanachama wa chama hicho wilayani hapa akiwamo Saimon Charles, wamesema wamefurahishwa na maandamano hayo ya amani, wakisema wamezunguka sehemu zote bila kusumbuliwa na mtu yeyote. 

Wakati huohuo, mkoani Dodoma chama hicho kilifanya maandamano ya amani yakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kuanzia Kisasa kupitia viwanja vya Bunge hadi Shule ya Sekondari Central.

Akizungumza na wafuasi wa chama hicho, Lissu  amesema hawaandamani kufanya mazoezi bali kudai Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi.

Amesema, viongozi wenzake wanaofanya maandamano lazima wawaeleze wanachama wao kwanini wanaandama, wasipofanya hivyo maana yake mikutano yao ya miaka yote haina tofauti na ya sasa.

“Itakuwa haina tofauti bali tofauti yake itakuwa ni kwanza kuanza kuchoshana barabarani, kabla ya kuja kwenye mkutano wa hadhara lazima tuonyeshe tofauti ya mikutano yetu ya siku zote na mikutano hii,”  amesema Lissu.

Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho, Peter Msigwa,  amesema wanataka Katiba mpya ili kuondoa tatizo la wateule wa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya watu waliochaguliwa na wananchi kinyume na Katiba ya nchi.

Amesema hivi sasa Mkuu wa Wilaya ana mamlaka zaidi ya mbunge ambaye amechaguliwa na wananchi, hali ambayo inapingana na Katiba.