Simba yafunguka hatima ya Phiri, atakiwa ajitume

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:09 AM Mar 28 2024
Mchezaji wa Simba SC Moses Phiri ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Power Dynamos ya Zambia.
Picha: Simba SC
Mchezaji wa Simba SC Moses Phiri ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Power Dynamos ya Zambia.

UONGOZI wa Simba umesema nyota, Moses Phiri, bado ni mchezaji wa timu yake kwa sababu ana mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja na alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya Power Dynamos ya Zambia.

Simba imesema hayo baada kuwapo na maswali mengi juu ya kuachwa kwa  mshambuliaji huyo katika kipindi cha dirisha dogo na Wekundu hao wa Msimbazi wakiwasajili, Freddy Michael na Pa Omar Jobe.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, alisema Phiri ni mchezaji halali wa Simba na alipelekwa kwa mkopo Power Dynamos kwa ajili ya kurejesha ubora wake na endapo ataimarika atarejea Msimbazi.

Kajula alisema uamuzi wa kumtoa kwa mkopo Mzambia huyo ulitokana na mapendekezo kutoka katika benchi la ufundi na hiyo ni hali ya kawaida pale mchezaji anaposhuka kiwango.

“Phiri ni mchezaji wetu halali ana mkataba wa mwaka moja, amepelekwa kwa mkopo Power Dynamos kwa lengo la kupata nafasi ya kucheza na kurudi katika ubora wake,” alisema Kajula.

Aliongeza baada ya nyota huyo kukosa namba katika kikosi cha kwanza baada ya kupona majeraha, alitakiwa kupambana ili kurudi kwenye ubora wake na kuisaidia timu hiyo.

Kajula aliwataja nyota mbadala wa Phiri waliosajiliwa ni Freddy na Pa Jobe ambao nao wanatakiwa kupewa muda wa kuzoea mazingira.

Simba inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwakaribisha Al Ahly katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.