DK. Shoo aonya matumizi mabaya ya fedha katika sharika

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:35 AM Mar 28 2024
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.
Picha: Maktaba.
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo.

ASKOFU wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, ameonya fedha za kanisa katika sharika zisitumike ndivyo sivyo.

Pia, amewahadharisha wachungaji wasikubali kuruhusu matumizi ya fedha mbichi ambazo hazijapita kwenye vitabu.

Alitoa angalizo hilo wakati wa kikao cha kwanza cha wachungaji zaidi ya 300 kutoka majimbo matano ya dayosisi hiyo, ambayo ni Kilimanjaro Mashariki, Kilimanjaro Kati, Hai, Siha na Karatu.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine, kilikuwa kinalenga kuwakumbusha kuwa waadilifu katika masuala ya fedha, kazi na mienendo ya maisha.

“Kuna taarifa za fedha za usharika kutumika ovyo, labda unakuta mchungaji anatumia nafasi yake kushawishi watu wasiokuwa waadilifu na wasiojua wajibu wao katika Baraza la Usharika.

“Unakuta mchungaji anasema hebu nipe Sh. 100,000 hapo, pesa ambayo ni mbichi haijapita kwenye vitabu. Unapofanya hivyo ni kukosa uaminifu na unafundisha wale wengine. Hii haina baraka, taratibu za utunzaji fedha zifuatwe.”

Aidha, Askofu Dk. Shoo, aliwasihi wachungaji hao kuendelea kutunza maadili ya utumishi.

 “Ndugu zangu wachungaji, tumeitiwa huduma hii takatifu kwa neema ya Mungu. Ninawakumbusha na kuwasihi sana, tutunze maadili ya utumishi na haya yanaanzia na wewe mwenyewe unavyoonekana. 

“How you behave (muonekano wako ulivyo), usionekana kama mchungaji wa kijiweni au mtu wa kijiweni, tafadhali!

…Utumishi huu una heshima yake, maneno yako unayozungumza yatofautiane na maneno ya kijiweni; lakini tutunze maadili ya wito wetu.” alisema.

Kwenye hotuba yake, Askofu Dk. Shoo aliwataka wachungaji kuwa waadilifu katika masuala ya fedha na kuweka kumbukumbu za fedha kwa uadilifu na kufuata taratibu.

Katika hatua nyingine, Askofu Dk. Shoo alisema katika majira haya ya kipindi cha kwaresma kila mmoja ajitafakari kuhusu jambo hili linalohusu maadili ya wito wao.