Mbarawa: Mv Mwanza kuanza kazi Juni

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 01:18 PM Mar 29 2024
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa.

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amehitimisha hatua ya mwisho ya majaribio ya safari ya meli ya Mv.Mwanza ‘Hapa kazi tu’ na kujiridhisha kuwa ifikapo Juni mwaka huu itaanza kazi rasmi.

Aliyasema hayo jana wakati wa safari ya majaribio ya meli hiyo katika Ziwa Victoria, kueleza kuwa wakati wa majaribio hayo imeendeshwa kwa kasi inayohitajika na kuonesha uwezo wa mkubwa kama inavyohitajika.

Alisema meli hiyo inayogharimu Sh. bilioni 127.27 inatarajiwa kukabidhiwa Mei 31 na baada ya hapo kuanza kazi za majaribio Juni mwaka huu endapo hakutakuwa na kikwazo.

“Tumeanzia kasi ya noti 10 mpaka noti 15 na wakati wote injini na mitambo yote ilikuwa ikifanya kazi vizuri bila tatizo lolote, hivyo kutokana na sisi kuthamini usalama kwanza tunajitahidi kuhakikisha ipo salama ili iweze kuwahudumia Watanzania kama ilivyopangwa,” alisema Prof.Mbarawa.

Alisema meli hiyo inatarajiwa kurahisisha shughuli za usafirishaji mizigo pamoja na kupunguza gharama za usafiri katika Ziwa Victoria na kutaja usafirishaji wa majini kuwa chini kulinganisha na usafiri mwingine.

Prof. Mbarawa alisema sasa serikali haitegemei kumuongezea muda wa utekelezaji wa mradi, bali kwa sasa wanashughulikia ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya bandari zinazotarajiwa kuhudumiwa na meli hiyo nchini, ikiwemo Bandari ya Kemondo Kagera pamoja na Mwanza Kaskazini.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Erick Hamis alisema kukamilika kwa majaribio hayo kunaongeza asilimia tatu katika utekelezaji wa meli hiyo na kufikia asilimia 96.

Alisema asilimia nyingine nne zinazosalia zinahusiana na uwekaji wa samani ndani ambazo ni pamoja na viti, meza, vitanda, kabati, kapeti pamoja na umaliziaji wa kawaida ambako vyote hadi ifikapo Mei 31, mwaka huu vitakuwa tayari.

Meneja Mradi, Luteni Kanali Vitus Mapunda alisema licha ya mradi huo kuelekea kukamilika kwa asilimia 100, utekelezaji wake ulikumbana na changamoto mbalimbali kutokana na meli hiyo kuwa ya kwanza kwa ukubwa kutengenezwa Tanzania na ukanda wa maziwa makuu, hivyo iliwachukua muda kupata mafunzo kadhaa kutoka kwa wahandisi wa Korea.

Nahodha wa meli hiyo wakati wa majaribio Kapt. Bembele Ng’wita alisema katika majaribio hayo ya siku tatu kila kifaa kinachotumika kwenye meli hiyo hususani katika mitambo ya uendeshaji kilijaribiwa na kuhakikisha vyote vinafanya kazi katika hali inayohitajika.