Wabunge wakunwa na majaribio SGR

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 01:09 PM Mar 29 2024
Makamu Mwenyekiti wa PIC, Augustine Vuma akizungumza na wandishi wa habari.

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na majaribio yanayoendelea ya treni ya umeme katika reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Akizungumza jana baada ya majaribio hayo, Makamu Mwenyekiti wa PIC, Augustine Vuma, alisema kamati hiyo pia imejiridhisha kuwa thamani ya fedha zilizotumika katika mradi huo zimetumika sawa na hatua za manunuzi zilifuatwa.

“Napenda kuipongeza serikali kwa kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha mradi unakamilika. Shughuli zitakapoanza, mradi huu utapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kwa asilimia 40.

“Natoa wito kwa uongozi wa TRC kuulinda mradi huu na kuhakikisha unakuwa endelevu. Pia  tunautaka uongozi wa TRC kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi kwa wakati kulingana na makubaliano ya kimkataba," alisema.

Vuma aliongeza kuwa mradi huo umetoa ajira za moja kwa moja 30,000 na ajira 150,000 zisizo za moja kwa moja hadi sasa hivyo jamii ina jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu yote inalindwa.

 Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Ally Karavina, alisema majaribio yanayoendelea yamezingatia taratibu zote za uhandisi.

“Tutatekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha shughuli hizo zinaanza mwishoni mwa Julai mwaka huu,” alisema.


 Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, aliwahakikishia wananchi kuwa shughuli hizo zitaanza mwishoni mwa Julai, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kutangaza gharama za nauli kama ilivyoelekezwa na serikali.

 Alisema majaribio kutoka Morogoro hadi Dodoma yataanza wakati wowote mwezi ujao na kuongeza kuwa wahandisi walikuwa wakikamilisha baadhi ya mitambo ili kuruhusu treni hiyo kupita.