Prof. Mkumbo: Umri wa kuishi umeongezeka

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:17 AM Apr 18 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ametaja mambo kadhaa ya kujivunia katika miaka 60 ya Muungano ikiwamo kuongezeka wastani wa umri wa kuishi kwa watanzania kutoka miaka 32 hadi 66 huku wanawake wakionekana wakiishi miaka mingi kuliko wanaume.

Akizungumza  na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Prof.Mkumbo amesema ustawi wa wananchi na nchi umeimarika ndani ya miaka 60 ya Muungano na  wastani wa umri wa kuishi kwa watanzania umeongezeka kutoka wastani wa miaka 32 wakati wa Muungano hadi kufikia miaka 66 mwaka 2022 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Mwaka 2022 na kwamba ifikapo mwaka 2025 inatarajiwa kufikia miaka 68.

Amefafanua kuwa katika sensa hiyo imeonesha wanawake wanaishi miaka mingi ambapo umri wao wa kuishi umefikia wastani wa miaka 68  kuliko wanaume ambao ni miaka 64.

Ameeleza kuwa kuongezeka kwa umri huo kumetokana na nchi imepiga hatua katika kuhakikisha Muungano unakuwa na hai na unadumu sambamba na kulinda na kudumisha amani, utulivu na mshimano ambao ni msingi wa maendeleo huku usalama wa chakula umeongezeka kutoka asilimia 60 ambao kwa sasa ni asilimia 124 wakati lengo likiwa ni kufikia asilimi 130 ifikapo mwaka 2025.