Shirika lakarabati miundombinu ya maji Hanang'

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 02:18 PM Apr 18 2024
Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Bi. Anna Mzinga akikabidhi nyaraka za makabidhiano ya mradi wa maboresho ya chanzo cha maji Nangwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Almishi Issa.
Picha: Beatrice Shayo
Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Bi. Anna Mzinga akikabidhi nyaraka za makabidhiano ya mradi wa maboresho ya chanzo cha maji Nangwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Almishi Issa.

SHIRIKA WaterAid limekamilisha ukarabati wa miundombinu ya chanzo cha maji iliyoathiriwa na maporomoko ya matope, mawe na magogo katika eneo la kata ya Nangwa, wilayani Hanang' mkoani Manyara, kwa gharama ya Sh. milioni 127.4.

Desemba 3, mwaka jana katika Wilaya ya Hanang' yalitokea maporomoko ya tope yaliyoambatana na mawe, magogo na maji kwa wingi kutoka mlima Hanang’ kuelekea makazi ya watu. 

Maafa ambayo hayakuwa mafuriko ya maji kama ilivyozoeleka na kusababisha madhara mbalimbali ukiwamo uharibifu wa miundombinu ya maji katika kata nne ambazo ni Gendabi, Jorodom, Nangwa na Gitting. 

Akizungumza katika hafla ya makabidhino ya mradi huo jana mkoani Manyara, Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, alisema  baada ya maporomoko yale walilazimika kufika kusaidia kurejesha huduma ya maji.

Amesema WaterAid ikiwa ni moja ya wadau wakuu wa masuala ya maji na usafi waliitikia kwa ukubwa na kukarabati miundombinu ya chanzo cha maji iliyoathirika na kusababisha wakazi 26,900 kupata huduma tena.

“Kufuatia changamoto hii iliyoikuta wilaya ya Hanang' mnamo mwishoni wa mwaka 2023, ilitupelekea sisi kuwa hapa kwasababu ili maisha ya mwanadamu yawe na utu na stara, tunaamini anapaswa kuwa na huduma za maji safi na salama pamoja na choo bora," amesema.

"Tulisukumwa sisi kama shirika linalotekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira, kukarabati chanzo hiki cha maji cha Nangwa ambacho kiliharibiwa vibaya sana na mvua kubwa,"

Amesema mbali na ukarabati wa chanjo cha maji,  Shirika la WaterAid lilitoa elimu ya usafi wa mazingira na vyoo bora katika ngazi ya kaya kwa watoa huduma za afya, wenyeviti wa kata na vijiji ili jamii kuwa na utayari wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.