Kilio hiki kikokotoo mafao ya wastaafu kifike mwisho

Nipashe
Published at 08:11 AM Apr 10 2024
Katuni.
Mchoraji: Abdul Kingo
Katuni.

KILIO cha kikokotoo cha mafao kwa wastaafu kimeendelea kusikika kila kona kutoka kwa wafanyakazi kupitia vyama vyao na vyama vya siasa.

Kwa sasa kimegusa wabunge ambao ndio waliopitisha sheria hiyo ambayo kwa sasa inaonekana kuwa kandamizi kwa wastaafu.     

Katika mkutano wa Bunge la Bajeti unaoendelea jijini Dodoma, sakata la kikokotoo hicho limeibuliwa na baadhi ya wabunge huku wakieleza machungu waliyoyapata wastaafu.

Wabunge hao waliochangia hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 24/25, wameinyooshea serikali kuwa ni kiini cha tatizo hilo.

Wabunge hao wamesema tatizo hilo kwa sasa ni kubwa tofauti na ahadi iliyotolewa na serikali kuwa wafanyakazi wameboreshewa mafao. Kinyume chake, walisema kikokotoo hicho kina madhara makubwa kwa wastaafu, hivyo ni vyema kamati ikaundwa ili kupata ufumbuzi wa haraka. 

Mmoja wa wabunge hao, Mrisho Gambo (Arusha Mjini - CCM), wakati akichangia hotuba ya makadirio hayo, pamoja na kushauri kuwapo suluhu ya jambo hilo, alisema kuna kilio cha wafanyakazi kila kona.   

Alisema katika uchunguzi wake kwa miaka 10 iliyopita, amebaini kwamba kikokotoo cha zamani kilikuwa bora kuliko cha sasa na hicho ndicho Watanzania wengi wanakitaka. 

Kwa mujibu wa kikokotoo hicho, mfanyakazi anapostaafu alikuwa anachukua asilimia 50 ya mafao yake na kuendelea kupata mafao kwa miaka 15.5. Kikokotoo cha sasa mfanyakazi anapostaafu anapata mafao ya mkupuo asilimia 33 na kuendelea kulipwa kwa miaka 12.5 tu. Pia kikokotoo hicho kimepunguzwa kutoka 1/540 na sasa ni 1/580 na kimechukua wastani wa mshahara wa miaka mitatu iliyo bora badala ya 10 iliyokuwa katika kile cha awali.

Kutokana na mfumo huo mpya wa ukokotoaji mafao, mbunge huyo amekwenda hatua zaidi, amebaini kuwa kwa kikotoo cha awali cha zilizokuwa PSSF ma LAPF, mfanyakazi aliyekuwa akilipwa mshahara wa Sh. 800,000 kwa mwezi alikuwa anapata mafao ya mkupuo ya Sh. 57,466,666 na kwa kikokotoo cha sasa ni Sh. 28,675,862. 

Pamoja na kuwapo kwa tofauti hiyo ya Sh. 29,190,804 mfanyakazi wa sasa anayestaafu anapata Sh. 388,137 badala ya Sh. 401,000 ya malipo ya kila mwezi. 

Kutokana na ukweli huo na bila kuuma maneno, mbunge huyo aliweka bayana kwamba katika hali ya kawaida kwenye kikokotoo hicho, yamefanyika makosa makubwa ambayo kwa sasa yanaumiza wafanyakazi ndiyo maana wameamua kuwatumia wabunge kwa kuwa ndio waliopitisha.

Hoja hiyo kwa nyakati tofauti, imeungwa mkono na wabunge wengi wakiwamo Ester Bulaya (Viti Maalumu – CHADEMA), Issay Paulo (Mbulu Mjini CCM) na Nicodemus Maganga (Mbogwe – CCM) ambao  licha ya kueleza kuwa wanapokea ujumbe kutoka kwa wastaafu kuhusu maumivu ya kikokotoo hicho, wamesisitiza kurudi katika meza ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi kukipitia upya.

Wahenga wanasema mwenye uchungu ni aliyefikwa na janga. Msemo huo unasadifu kilio cha kikokotoo kwa wastaafu baada ya kuonja shubiri na maumivu baada ya kupokea mafao hayo. 

Jambo lingine linalotia uchungu ni baadhi ya kauli za viongozi wa serikali kwamba lengo la kikokotoo hicho ni kuwatunzia fedha wastaafu kwa madai kuwa wanaweza kutumia vibaya na kupata taabu baadaye. Serikali inapaswa kutambua kwamba wafanyakazi hao wametumika kwa zaidi ya miaka 30 hadi 40 na wanahitaji kufaidi matunda yao ya utumishi lakini sasa wanaumia kutokana na kutotimia kwa ndoto zao kuhusu kupata mafao manono baada ya utumishi wao kukoma.    

Kuna msemo kwamba kuteleza si kuanguka, hivyo ni vyema serikali, kama inavyojinasibu kwamba ni sikivu, irejee mezani na vyama vya wafanyakazi ili kuona njia nzuri ya kurekebisha jambo hilo na hatimaye kuwafuta uchungu wa moyoni wafanyakazi hawa ambao wamelitumikia taifa kwa uaminifu mkubwa. Ni vyema kilio hiki sasa kikafika mwisho.