Mabilioni yaliyotengwa kuwakopesha wajasiriamali yalete matokeo chanya

Nipashe
Published at 10:17 AM Apr 11 2024
Bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali.
Picha: Maktaba
Bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali.

WAJASIRIAMALI wadogo nchini wametangaziwa neema kutokana na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kutenga Sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha ili kupanua wigo wa ajira na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2024.

Hatua hiyo ni ya kupongezwa na ya kupigiwa mfano kwa sababu kwa idadi ya walengwa 2,000 katika mpango huo ni dhahiri kwamba kutakuwa na matokeo chanya katika biashara. Kuwawezesha wafanyabiashara wadogo ndio msingi mkuu wa ukuaji wa biashara na uchumi katika taifa lolote ndiyo maana kuna msemo kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha.

Msemo huo unasadifu na mpango huo wa TCB katika kukuza uchumi wa nchi kwa sababu mara nyingi watu wamekuwa wakilalamika kuwa kikwazo cha kufanya biashara kwao ni ukosefu wa mitaji, sasa fursa imepatikana kwa hiyo wale wanaokidhi vigezo na masharti hawana budi kukichangamkia.

Kama alivyosema Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Muhayo, wajasiriamali wadogo wanachangia asilimia 30 katika ukuaji wa uchumi, ni wazi kwamba kuwapo kwa fursa hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Uchumi katika ngazi za familia kwa kuwa wajasiriamali hao watajiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi. Kwa maneno mengine, umaskini wa hali na wa kipato utapungua miongoni mwa Watanzania kupitia wajasiriamali hao. 

Hakika TCB imeona mbali kwa kuwawezesha wajasiriamali hao kwani ndio mpango mzima katika maendeleo ya biashara kutoka wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa ambao mwisho huwa wafanyabiashara wakubwa na maarufu ambao pia ni tegemeo kubwa katika ulipaji kodi na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. 

Katika historia ya wafanyabiashara duniani kote, hakuna aliyezaliwa akiwa milionea au bilionea bali wote walianza katika hatua za chini huku wakikuza mitaji yao na kupanua biashara kulingana na fursa zilizokuwa na zinazoendelea kujitokeza.  

Kwa mantiki hiyo, kutafungua fursa nyingi za kibiashara hasa uzalishaji na kuongeza thamani kama lengo la uwezeshaji huo. Pia kuwezeshwa kwa wajasiriamali hao kutasaidia kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania kwa kuwa biashara zao zinapokua, watakuwa na uwezo wa kuajiri watu kusaidia shughuli na ukuaji wake na pia ongezeko la bidhaa na mzunguko wa fedha. 

Pamoja na ukweli huo, ni wakati sasa kwa wajasiriamali wadogo kuchangamkia fursa hiyo na kutekeleza kwa vitendo katika uzalishaji mali na hatimaye kupanua mitaji na wigo wa biashara kwa ujumla. Hiyo inatokana na ukweli kwamba kilio chao kuhusu mitaji kimesikika baada ya benki hiyo kutangaza kuwa imetenga mabilioni hayo.

Suala lingine ambalo wajasiriamali hao wanapaswa kuzingatia ni uaminifu katika matumizi ya fedha hizo kwa lengo lililokusudiwa kwa kufanya biashara badala ya kuchepusha na kufanya mambo mengine kama sherehe, kununua nguo na samani na hata kuoa wake wa nyongeza. 

Wajasiriamali hao pia wanapaswa kuwa waaminifu kama urejeshaji wa fedha hizo kwa sababu hazijatolewa kama hisani wala msaada bali mikopo, hivyo wanatakiwa kuheshimu mikataba ya upatikanaji wake. 

Kwa muda mrefu, uzoefu unaonyesha  kwamba baadhi ya watu wanapopata mikopo kutoka taasisi za fedha, hawazitumii kwa malengo yaliyokusudiwa bali huzielekeza kwenye sherehe, ndoa na kununua vitu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Pia baadhi ya wakopaji wamekuwa hawarejeshi mikopo kama mikataba inavyoelekeza hadi wakopeshaji kuchukua hatua za kuwatangaza kupitia vyombo vya habari, kupokwa mali na kupigwa mnada.

 Ni vyema wahusika wa mabilioni hayo yaliyotengwa na TCB yakatumika na wajasiriamali kwa malengo kusudiwa ili kuwawezesha kukuza biashara na kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuchangia ukuaji wa Uchumi kwa ujumla.