Usafiri treni ya umeme utumike kuleta mageuzi sekta ya uchukuzi

Nipashe
Published at 01:10 PM Mar 29 2024
Treni ya umeme ikiwa katika majaribio kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Picha: Ikulu.
Treni ya umeme ikiwa katika majaribio kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.

SEKTA ya usafirishaji ni muhimu katika kukuza uchumi na vilevile mageuzi ya maendeleo nchini.

Usafiri unapokuwa wa uhakika na kuaminika huvutia pia wafanyabiashara wa mataifa mengine kuutumia.

Usafiri wa treni ya kisasa inayotumia umeme, unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa nchini utakapoanza rasmi kutumika.

Jambo la kwanza utaokoa muda mwingi kwa wasafiri kukaa barabarani kufika wanakokwenda na vilevile utaokoa uharibifu wa miundombinu ya barabara pale malori yanapobeba mizigo mizito.

Hivi karibuni Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na majaribio yanayoendelea ya treni ya umeme katika reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma, amesema kamati hiyo pia imejiridhisha kuwa thamani ya fedha zilizotumika katika mradi huo zimetumika sawa na hatua za ununuzi zilifuatwa.

Hata hivyo, ombi la Kamati hiyo ni kuutaka uongozi wa TRC kuulinda mradi huo ili kuhakikisha unakuwa endelevu, pia kamati hiyo imetaka mkandarasi kukamilisha mradi kwa wakati kulingana na makubaliano ya kimkataba.

Mradi huo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, umetoa ajira za moja kwa moja 30,000 na ajira 150,000 zisizo za moja kwa moja hadi sasa na kwamba jamii ina jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu yote inalindwa.

Mwenyekiti amekumbusha jambo la msingi la jamii kulinda miundombinu ya mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta faida nchini.

Kwa watu ambao wameshasafiri katika nchi zingine duniani zinazotumia usafiri huo, watakubaliana na mwenyekiti kuhusu jamii kulinda miundombinu hiyo.

Uharibifu mara kwa mara hufanywa na jamii kwa kutokuwa na uzalendo au kuhujumu miundombinu kwa makusudi.

Hili linaonekana hata kwenye barabara za kisasa zilizojengwa nchini kwa uharibifu unaofanyika kung’olewa kwa kingo za madaraja na alama za barabarani kwa lengo la kuchukua vyuma na kwenda kuviuza kama vyuma chakavu.

Miradi kama hii inalindwa kuanzia njia zinazotumika mpaka vyombo vinavyobeba abiria. Kwa mfano kwenye baadhi ya nchi ambazo zinatumia usafiri wa treni kama wa umma, kuna masharti yanayokataza abiria kula au kunywa aina yoyote ya kinywaji anapokuwa ndani ya usafiri huo.

Abiria yeyote atakayekwenda kinyume na onyo hilo anatozwa faini kubwa na sheria inatekelezwa.

Msafiri yeyote awe mwenyeji au mgeni ni lazima anapoingia kwenye usafiri huo asome masharti kuepuka kupigwa faini.

Hatua hiyo imesaidia watu kufuata sheria na vilevile kuwa wasimamizi wa wengine wanaojisahau.

Hapa nchini pia hilo linawezekana kama kutakuwa na ufuatiliaji na utekelezaji ili kulinda miradi hiyo mizuri itakayosaidia nchi kuongeza mapato.

Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Ally Karavina, amehakikisha kuwa majaribio yanayoendelea yamezingatia taratibu zote za uhandisi.

Habari njema ni kuwa shughuli hizo zinaanza mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amewahakikishia wananchi kutangaza gharama za nauli kama ilivyoelekezwa na serikali.

Majaribio kutoka Morogoro hadi Dodoma yataanza wakati wowote mwezi ujao na wahandisi walikuwa wakikamilisha baadhi ya mitambo ili kuruhusu treni hiyo kupita.