Giza hili kuelekea Daraja la Magufuli linatukwaza abiria kwa usalama wetu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:16 PM Apr 18 2024
KITUO cha Mabasi cha Magufuli.
PICHA: MAKTABA
KITUO cha Mabasi cha Magufuli.

KITUO cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi, mkoani Dar es Salaam, kinatoa huduma za safari ziendazo mikoani na nchi jirani, huku kikitajwa kuwa na hadhi ya Kimataifa.

Hiyo inatokana na idadi ya huduma inazotoa kwa siku kwa ruti tofauti kwenda maeneo tofauti na Mabasi yanayokadiriwa kufikia 200 kwa siku.

Kwa sasa, unapoingia au kutoka kwenye kituo hicho kwa abiria wanaotembea kwa miguu inawalazimu kupita njia ya daraja la juu, ili kuwapa usalama watumiaji wa kituo hicho hususan abiria.

Uwapo wa giza kwenye daraja hilo hasa kwa watumiaji wa usiku imekuwa changamoto, kwa kuwa wanaolitumia iwe ni watu wenye ulemavu, wazee, watoto na makundi mengine ni hatari kwao.

Hata kwa usalama, pia inakuwa ni mdogo ikizingatiwa kwamba juu ya daraja kumezungukwa na wapiga debe ambao wao kazi yao ni kushawishi abiria watumie usafiri wao, lakini nani anajua kwamba wote kazi yao ni hiyo.

Kwenye msafara wa mamba na kenge wamo, huo ni msemo wa waswahili ambao naweza kuutumia hapa, kwa kuwa wapiga debe hao mbali na kukatazwa na mamlaka husika kufanya hivyo, kuna ushahidi unaotolewa mara kadhaa kwamba wapo na vibaka.

Giza hilo kwenye daraja hili isiwe fursa kwa watu wenye nia ovu na kutaka kuutumia mwanya huo kwa kuleta usumbufu kwa watumiaji hasa abiria.

Kama ambavyo inafahamika kwamba matumizi ya kituo hicho ni saa 24, kwa kuwa wapo wasafiri wanaotoka kanda mbalimbali ikiwamo ya Ziwa ambao huwasili kituoni zaidi ya saa sita usiku.

Mazingira rafiki ya kituo hiki yatakifanya kituo hicho kuwa salama kwa mtu yeyote hasa wageni na majira yeyote, mchana au usiku kwa kuwa, ni wakati wa mamlaka husika kuzingatia uwepo wa taa eneo hili.

Wakati mazingira ya watumiaji wa kituo hicho kuwalazimu abiria kupita juu ya daraja ni vyema eneo liwe na uhakika wa kulitumia daraja hilo, kwa kuweka taa na watu ambao hugeuza eneo hilo kijiwe wapigwe marufuku.

Kwa ilivyo sasa matumizi ya taa sio ya gharama, kwa kuwa kuna taa zilizoundwa kwa kutegemea chanzo cha jua mchana kutwa, kisha usiku taa zikawashwa bila gharama ya umeme utokanano na gharama za Tanesco.

Pia, daraja hilo lifanyiwe usafi kwa kuwa mara kadhaa usafi huwa duni, hujaa mchanga, taka za plastiki na makaratasi, uchafu ambao unashusha hadhi ya kituo hicho ambacho ni taswira ya mkoa na nchi kutokana na kupokea wageni wanaotoka nchi jirani kila uchao.

Kituo hicho kilizinduliwa Februari mwaka 2021 na Hayati John Magufuli, huku kikiwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 3,456 kwa siku, abiria 224,000 kwa siku na kuegesha magari madogo zaidi ya 280 na kuegeshwa mabasi 1000 wakati wa usiku.

Kadhalika, ofisi za mabenki, huduma za simu, hoteli, Ofisi za Uhamiaji, maduka pamoja na eneo la kupumzikia abiria na maliwato ni kati ya huduma muhimu zinazopatikana kituo hicho.