Kocha Pamba ataka fungu la usajili Ligi Kuu mapema

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:51 AM May 09 2024
Kikosi cha Pamba FC.
Picha: Maktaba
Kikosi cha Pamba FC.

KOCHA Mkuu wa Pamba FC, Renatus Shija, amependekeza uongozi wa klabu hiyo kuanza maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao mapema kwa kutoa fungu kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya, pamoja na kuwalinda waliopo wasiondoke huku akiwataka mashabiki wa soka Mwanza kuwa watulivu.

Akizungumza juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, baada ya kumalizika mechi maalum ya kuikabidhi KenGold ubingwa wa Championship, kocha huyo alisema Ligi Kuu Tanzania kwa sasa imebadilika kwani ina ushindani mkubwa, hivyo maandalizi ya mapema  yanatakiwa ili kuifanya Pamba kuwa timu ya ushindani.

"Tumeshapanda Ligi Kuu, huu sasa siyo wakati wa maneno maneno, wakazi wa Mwanza watulie, Pamba inahitaji maandalizi ya mapema, tunakwenda kwenye Ligi Kuu huko ushindani ni mkubwa zaidi, menejimenti iweke fungu la usajili, pamoja na la kuwalinda wachezaji kwa sababu ushindani ni mkubwa wa kugombea wachezaji.

"Hatuwezi kuingia moja kwa moja na kuweka ushindani mkubwa moja kwa moja, lazima kwanza tuizoee ligi," alisema kocha huyo aliyepandisha Pamba kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23.

Katika mechi hiyo, timu hizo ambazo zote zimepanda Ligi Kuu, zilitoka sare ya bao 1-1 na KenGold kupewa kombe lao.

Wakati huo huo, Kocha Kengold,  Jumanne Chale ameonekana kuwa na wasiwasi na kibarua chake.

Beki huyo wa zamani wa RTC Kagera, alisema anasikia maneno maneno kuwa huenda asiendelee kuifundisha timu hiyo, badala yake ataletwa kocha mwingine.

"Huenda nisiendelee kuwa katika timu hii, au hata nikiendelea nitakuwa kocha msaidizi, lakini ndiyo soka lilivyo, nakiri kabisa kuwa hayo maneno yapo, lakini hayawezi kunifanya mimi nisiendelee kufundisha soka, mimi najua ninachofanya," alisema kocha huyo.