Simba, Azam vita ya nafasi ya pili

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:39 AM May 09 2024
Wachezaji wa Simba wakishangilia goli katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu.
Picha: Mtandaoni
Wachezaji wa Simba wakishangilia goli katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu.

NYASI za Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam leo zitawaka moto katika mchezo wa kusaka heshima na nafasi ya kukata tiketi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Azam FC leo wanakuwa nyumbani kuwakaribisha Simba, kwenye uwanja huo mchezo utakaochezwa saa 12:15 jioni huku timu zote zikihitaji matokeo katika mchezo huo.

Simba wako nafasi ya tatu wakiwa na alama 53 ikiwa na mchezo mmoja mkononi huku wakiwa chini ya Azam kwa tofauti ya pointi nne huku Wanalambalamba hao wakishika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga.

Katika mchezo wa leo timu zote zinahitaji kupata matokeo chanya na endapo timu yoyote itaibuka na ushindi itajiweka kwenye mazingira mazuri ya kumaliza nafasi ya pili na kuendelea kutoa msukumo kwa Yanga kwenye kuwania ubingwa msimu huu.

Kama Simba ikipoteza mechi ya leo itajiweka kwenye nafasi ngumu ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya misimu zaidi ya mitano.

Katika michezo 18 waliyokutana timu hizo, Simba imeshinda mara sita, imepoteza tatu na Azam FC imepata matokeo mara tatu na kupoteza sita, wote wametoka sare mara tisa.

Kuelekea mchezo huo wa leo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema maandalizi ya mchezo wa leo yamekamilika na wapo tayari kushindana kupata matokeo mazuri.

Alisema wanatambua Azam ni timu nzuri yenye kutoa ushindani lakini wamejipanga kufanya vizuri na kuondoka na pointi tatu.

“Siku zote mchezo wa mpira kuna makosa hayakwepeki, kikubwa ni kuyafanyia kazi katika uwanja wa mazoezi, mechi iliyopita tulifanya makosa naamini tumesahihisha na kuyapunguza tayari kwa mchezo wa leo.

"Soka ni mchezo wa wazi hakuna kuficha, tunaingia uwanjani kusaka pointi tatu ambazo ni muhimu sana, leo tutaendelea kumkosa Chama (Clatous) ambaye ni majeruhi na anatumikia adhabu, Miquison, Ntibazonkiza, Onana wote ni majeruhi pia, lakini hiyo sio tatizo kwa kuwa wachezaji waliopo ni waajiriwa wa Simba atakayepewa jezi atatakiwa kutumikia timu na kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Mgunda. 

Mchezaji wa Simba kwa niaba ya wachezaji wenzake, Hussein Kazi alisema wapo vizuri na wanatambua umuhimu wa mchezo wa leo na kuhakikisha wanapambana kusaka pointi tatu muhimu.

Kwa upande wake, Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry alisema mara ya mwisho walikutana na Simba katika mashindano ya Muungano na kupoteza, hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari wakitaka pointi tatu.

Alisema wamejipanga vizuri, wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na kusaka pointi tatu muhimu mbele ya wapinzani wao kwa ajili ya kufikia malengo yao.

“Ni mechi ya ushindani mkubwa, Simba wako vizuri, tumefanya maandalizi mazuri na wachezaji wapo tayari kwa mchezo, naomba waamuzi kuwa waungwana kwa sababu maamuzi mengi yamekuwa yakiharibiwa, wawe makini ili uwe mchezo wa haki,” alisema Bruno.

Nahodha wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda alisema wanataka kulipa kisasi cha kufungwa kwenye mashindano ya Muungano, watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.

“Mchezo wa kesho (leo ) ni muhimu kwa kila timu kwa sababu ya kila mmoja wetu anataka pointi kulingana na jinsi alama tulizopishana, tunawafahamu Simba na wao wanatufahamu pia, utakuwa mchezo mgumu, tunapaswa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu,” alisema Lusajo.