Yanga yaweka dau mezani

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:32 AM May 09 2024
Kibu Denis.
Picha: Simba SC
Kibu Denis.

YANGA ni kama imeamua kujiimarisha zaidi kwa ajili ya msimu ujao, inaelezwa chini ya Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, wameanza mazungumzo na nyota wa Simba, Kibu Denis.

Mkataba wa mchezaji huyo na Simba unaisha mwishoni mwa msimu huu ingawa Simba wanataka kumbakisha mchezaji huyo, taarifa zinasema tayari uongozi wa Yanga umeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kumsajili nyota huyo.

Inaelezwa Yanga wameweka mezani ofa ya shilingi milioni 150 pamoja na gari kwa mchezaji huyo wa zamani wa Mbeya City na tayari uongozi wa Yanga upo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo.

Imeelezwa kuwa ofa waliyoweka Yanga ni Sh. milioni 150 na gari ikiwa ni sehemu ya ofa yao ya kumuhitaji nyota huyo ambaye mkataba wake unafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa zilizopatikana jana mchana zinasema viongozi wa Yanga wameanza mazungumzo na nyota huyo na kuweka ofa hiyo mezani lakini Kibu hajatoa tamko lolote la kukubali au kukataa ofa hiyo iliyokwa mezani na mabosi wa Yanga.

Mtoa taarifa amesema Kibu ameingia katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa na Yanga baada ya Kocha Miguel Gamondi kutaka kuongezewa mshambuliaji mzawa kwa lengo la kuimarisha safu hiyo ya ushambuliaji.

“Licha ya kuwekewa ofa hiyo hadi sasa Kibu hajasema lolote kuhusu kukubali au kukataa, hii inatokana na kusubiria waajiriwa wake Simba kuhusu ofa yao, pia Azam FC nao wameonyesha nia ya kuhitaji huduma ya nyota huyo,” alisema mtoa taarifa hizo.

Alisema Simba nao hawajakata tamaa ya kumbakisha mchezaji huyo kwani nao wamemwekea ofa mezani mchezaji huyo.

"Sasa hivi Kibu ndio mwenye uamuzi kuamua wapi atie saini, ana ofa mbili za uhakika lakini pia Azam wameonyesha nia ya kumtaka pia," alisema mtoa habari huyo.

Aliongeza kuwa mchakato wa usajili unaendelea kwa kasi ndani ya Yanga, baada ya viongozi na benchi la ufundi linaloongozwa Gamondi kukubaliana kuachana na Agustino Okrah na nafasi yake kuchukuliwa na Prince Dube.

“Kuhusu Musonda (Kennedy) kuna uwezekano mkubwa Yanga kubadilishana na mchezaji kutoka TP Mazembe, Phillipe Kinzumbi, mazungumzo kati ya Hersi na Rais wa klabu hiyo ya nchini DR Congo yanaendelea,” alisema mtoa taarifa hizo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alibainisha kuwa wapo makini sana katika usajili na wanachokifanya ni kuanza kuangalia na kufanyia kazi mapendekezo ya awali ya benchi la ufundi katika usajili.

“Niwaambie kuwa tutawashangaza watu kwenye usajili ujao, kwa sababu tunahitaji msimu ujao tuendelee kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, wasubiri kuona kile viongozi wanachofanya,” alisema Kamwe.