Madereva wa daladala mnapogoma, hamuikomoi serikali bali wananchi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 01:31 PM Mar 15 2024
Abiria wakitaka kuingia kwenye daladala.
Picha:Mtandao
Abiria wakitaka kuingia kwenye daladala.

USAFIRI wa Daladala ni usafiri, ambao unatumiwa na rika mbalimbali kutoka sehemu fulani kwenda nyingine.

Kutokana usafiri huo kuwa tegemezi kwa jamii, sasa inatakiwa suala la kugoma kutoa huduma liangaliwe katika tafsiri pana. 

Hata kabla ya ndugu zetu wa daladala kugoma kutoa huduma hizo, wanatakiwa kuangalia ni kundi lipi ambalo litaathirika pale wanapogoma kutoa huduma ya usafiri huo. 

Usafiri huo sasa unatumiwa na wanafunzi, wafanyabiashara, watumishi kutoka sehemu mbalimbali na jamii. 

Kuwapo mgomo kunachangia kwa kiasi kikubwa wanaotumia usafiri huo kutofika kwa wakati katika maeneo wanayoenda, hasa makazini.  

Vilevile, kutofika kwa wakati katika maeneo wanayoenda, kunatokana na abiria kukaa vituoni muda mrefu huku wakisubiri usafiri, mara wanapata taarifa kama hizo za mgomo, hakuna usafiri na wanaanza kutafuta njia zingine za kuwafikisha maeneo wanayoenda. 

Kinachoshangaza, wenye daladala wanaingia barabarani na daladala zao wanazipaki, badala ya kuchukua abiria, wanacheka tu kila wanakopita vituo vya daladala na kukuta watu wamejaa wakisubiri huduma zao. 

Kutokana na kutambulika katika nchi yetu kuwa upo usafiri huo, lakini kuna taratibu zinazofanywa na wamiliki wa vyombo hivyo, baina yao na serikali. 

Inajukukana vyombo hivyo vina wawakilishi wao, ambao hata penye changamoto yoyote, wawakilishi huzungumza na serikali, ili kuhakikisha suluhu inapatikana. 

Pamoja na changamoto kutokea, madereva wa vyombo hivyo wakaamua kukimbilia uamuzi wa kugoma kutoa huduma ya usafiri, wakidhani kugoma kwao wanaikomesha serikali, kumbe mgomo unawaathiri watumiaji usafiri huo. 

Ilikuwa siku ya Jumatatu, Machi 11 wiki hii daladala za Mwanza zikagoma kutoa huduma ya usafiri kuanzia alfajiri kwa madai ya bajaji, zimekuwa nyingi na kuwafanya washindwe kufanya kazi zao vizuri. 

Tunajua biashara ni ushindani, hata kama bajaji nazo zinatoa huduma ya kusafirisha abiria, kuna vitu mnatakiwa kukaa meza moja na wenye, bajaji na sio kusitisha huduma. 

Ikumbukwe kuwa watu kutoka  alfajiri wanatumia daladala kwenda maeneo ya mijini na vijijini, ambako bajaji zinaweza kutofika katika maeneo hayo. 

Wapo watu wanatumia daladala kwenda katika vituo vikubwa vya mabadiliko yaendayo mikoani, ambao nauli hulipa ya kawaida. Lakini mnapogoma mnamfanya mtu kukodi bajaji kwa gharama kubwa kwenda kituo cha mabasi ya mikoani. 

Wapo wanaopanda daladala kwenda kufuata huduma za afya. Lakini kutokana na kugoma kwenu mnasababisha wananchi kukodisha bajaji kwa bei kubwa kwenda vituo vya afya kupeleka wagonjwa kupata huduma za afya. 

Mgomo huo unachangia watu kuingia gharama kubwa kukodi bajaji kwenda maeneo ambayo walitakiwa kufika kwa kutumia usafiri wa daladala. 

Bajaji zipo, lakini haziwezi kuchukuwa abiria wengi kwa wakati mmoja na badala yake, watakaowahi wataingia katika bajaji watalipia nauli kama ya daladala na watakapoona hawawezi kukaa vituoni watalazimika kukodi bajaji ili wafike sehemu wanazoenda. 

Kutokana na hali hiyo, bajaji na bodaboda ndio zinazopiga debe kubeba wananchi kuwapeleka mijini. 

Ieleweke, mgomo unawaathiri wanafunzi wanaolazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu, kwani hakuna pikipiki wala bajaji itakayowabeba kwa shilingi 200 za nauli zao. 

Hivyo, hii migomo mnayoifanya enyi mnohudumia daladala pasipo kuliangalia hilo kwa mawanda mapana, muelewe hamuiumizi serikali, bali wanaotumia usafiri huo.