Tuliwapokea wanafunzi wa Sudan, kwa nini isiwe Al Hilal kwenye Ligi?

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 04:38 PM Mar 23 2024
Wanafunzi wa Sudan.
PICHA: MILLARD AYO
Wanafunzi wa Sudan.

NAKUMBUKA Juni mwaka jana, Tanzania ilipokea kiasi cha wanafunzi 150 kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Khartoum nchini Sudan.

 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilithibitisha kupokea wanafunzi hao ambao waliomba kuendelea na masomo yao ya mwaka wa mwisho kwa vitendo katika hospitali jijini Dar es Salaam.

Mapigano ambayo yanaendelea nchini Sudan yanaendelea kusababisha maafa kwa maelfu ya raia wa taifa hilo kuikimbia nchi yao ambayo ndiyo yalisababisha wanafunzi hao kuwa miongoni mwa waathirika wa machafuko hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya taifa ya Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi akawahakikishia kuwa wamekuja sehemu sahihi na watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanamaliza masomo yao kwa salama na amani.

Ujio wa wanafunzi hao ulileta utani mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kama ilivyo kawaida ya Watanzania.

Watanzania ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii katika Bara la Afrika, ambapo wakati mwingine huitumia kwa kupeleka ujumbe kwa njia ya mzaha na utani kama ilivyo kawaida, na si kwa wagomvi, bali hupenda mijadala na utani. 

Hivi karibuni, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lilitangaza kuipokea timu ya mpira wa miguu ya Al Hilal kutoka huko huko Sudan na kwa sababu hizo hizo.

TFF ilitangaza kuingiza timu hiyo kwenye ratiba ya michezo ya Ligi Kuu msimu ujao japo matokeo yao hayataathiri msimamo wa ligi hiyo.

Baada ya kutangazwa hivyo na TFF, cha kushangaza baadhi ya mashabiki wa soka wameonekana kupinga mpango huo, wakidai ni kuidhalilisha Ligi ya Tanzania.

Hata sasa unashangaa, kwa nini sababu za kuwapokea wanafunzi ziwe sawa, lakini za timu ya mpira wa miguu ziwe si sawa?

Binafsi naona kinachofanyika ni kile kile, kuifanya timu hiyo kwanza wachezaji wake kukaa sehemu salama lakini pia kushiriki shughuli za kimichezo.

Timu hiyo imeomba kucheza ligi Tanzania ili wachezaji wake wawe fiti pale watakapokuwa wanakwenda kucheza mechi za kimataifa kwa sababu Sudan kwa sasa hakuna ligi na haijulikani vita itaisha lini.

Ndiyo maana si timu hiyo tu, hata waamuzi nao wamechukuliwa kwa ajili ya kuchezesha ligi msimu ujao. Nia ni ile ile tu kama ya wale wanafunzi.

Binafasi naipongeza TFF, Wallace Karia mwenyewe kama Rais, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo naamini kuwa kwa pamoja wamebariki hilo.

Ni kama wale wanafunzi, ambapo naamini Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilihusika katika mchakato mzima wa kuwapokea.

Ninachoshauri wakati wa kwenda kutengeneza kanuni za kuiruhusu Al Hilal kucheza Ligi kuu Tanzania Bara msimu ujao kusiwe na kona kona, ziongezwe timu ili kuwa 18, pamoja na yenyewe, lakini ipewe pointi tatu ikishinda na timu ikiifunga ipewe pointi tatu na hili lifanyike hadi mwisho wa msimu.

Baada ya hapo ikiwa ya kwanza, basi bingwa atakuwa yule aliyeshika nafasi ya pili, na ikishika moja kati ya nafasi nne za juu, timu ya tano ndiyo ihesabiwe moja kati ya timu nne za juu.

Binafsi siungi mkono eti ikishinda isipewe pointi au timu ikiifunga isipate pointi, hili si sawa.
 Ili kuipa nguvu Ligi ni lazima kuwe na ushindani, ikiwa ya kwanza ipewe pesa zake za mshindi wa kwanza, lakini isiwe bingwa wa nchi.