Serikali yasikia kilio kikokotoo

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:05 AM Apr 17 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
PICHA: MAKTABA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

KUTOKANA na kuibuka upya kwa mijadala mbalimbali ndani na nje ya Bunge kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo kipya cha mafao ya wastaafu, serikali imesema imepokea maoni yote yaliyotolewa na wadau pamoja na wabunge na kuahidi kufanyia kazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema hayo bungeni wakati wa kuhitimisha hoja ya makadirio ya Mapato na matumizi ya  Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/25.

Majaliwa amesema hoja zilizoibuliwa na wabunge wakati wa uchangiaji wa hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi, ikiwamo ya ulipaji wa mafao ya wafanyakazi kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii,  serikali imesikia na kupokea maoni mbalimbali ya wadau wakiwamo wabunge, wafanyakazi na vyama vya waajiri na wafanyakazi.

Amesema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wastaafu na itaendelea kufanya tathimini kwa kuzingatia sheria za kazi.

Pia amesema serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii ikiwamo mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali na waziri wa kazi na ajira kusimamia na kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha kuhusu.

Kuhusu hoja ya serikali kupunguza uhaba wa walimu ili kuendana na mitaala mipya ya elimu, iliyojibiwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya walimu pamoja na kutoa fursa mpya za ajira.

Amesema kwa mwaka 2023/24 serikali ilitoa nafasi za ajira 10,505 za walimu na kwa  mwaka 2024/25 inatarajia kufoa ajira mpya kwa walimu 10,590,  ili kutatua kwa kiwango kikubwa kero zilizoko katika eneo hilo.

Akizungumzia hoja ya serikali kuweka mikakati ya upatikanaji wa vyanzo vingi vya mapato ili kuwezesha bima za afya kwa wananchi wa vijijini, Waziri Mkuu amesema serikali inapokea mapendekezo yote na kuahidi kufanyiwa kazi.

Amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2023 imeanzisha mfuko kwa ajili ya kugharimia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na kubainisha vyanzo vya fedha vya mfuko huo na serikali itaendelea kupokea mapendekezo ya uendeshaji wa mfuko ikiwemo vyanzo vya mapato na kufanya maboresho kadri inavyofaa.

Kuhusu wanyamapori kuvamia maeneo ya wananchi mauaji ya watu kwenye hifadhi, Majaliwa amesema serikali inatambua madhara ambayo yamekuwa yakisababishwa na wanyamapori kuvamia makazi na mashamba na madhara kwa wananchi waishio karibu na hifadhi yakiwamo ulemavu, vifo na uharibifu wa mali.

Amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwamo utoaji wa elimu kukabiliana na wanyama waharibifu, uanzishaji wa vituo vya ulinzi kwa maofisa wanyamapori.

“Pia kuna changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina yao na askari wa hifadhi ambayo imekuwa ikisababisha vifo na wananchi kujeruhiwa na askari wa hifadhi,”amesema.

Waziri Mkuu amewakumbusha wasimamizi wa hifadhi kuzingatia taratibu wakati wa kushughulikia uvamizi hifadhini na kuwasihi wananchi kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuacha tabia ya kuingia hifadhini, kuingiza mifugo, kufanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi na uwindaji haramu.

Bunge  limepitisha makadirio ya Sh. bilioni 532.79 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/25 ikiwa  ni Sh.bilioni 350.988 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake na Sh. bilioni 181.8 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.