Israel yaapa kulipa kisasi dhidi ya Iran

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:37 AM Apr 16 2024
Baraza la vita la Israel lilifanya kikao kujadili hatua za kuichukulia Iran baada ya shambulizi lake la makombora na droni.
Picha: IDF/UPI/newscom/picture alliance
Baraza la vita la Israel lilifanya kikao kujadili hatua za kuichukulia Iran baada ya shambulizi lake la makombora na droni.

MKUU wa Majeshi ya Israel, Herzi Halevi ameapa kuchukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Iran baada ya shambulizi walilolifanya mwishoni mwa wiki. Iran ilirusha zaidi ya makombora 300 na droni kuelekea Israel Jumapili usiku.

Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha Channel 12 cha nchini humo, kimeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, jana usiku aliongoza kikao cha baraza la vita la serikali yake ambacho kilidumu kwa muda wa saa tatu na kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kujibu shambulizi hilo la Iran.  

DW imeripoti kuwa, hatua zilizojadiliwa na baraza hilo la mawaziri la vita zilianzia kwa zile ndogo hadi zile kali zaidi, na kwamba Israel inalenga kuweka usawa kati ya kusababisha uharibifu nchini Iran lakini sio kuzusha vita vya kikanda, huku Mshirika mkuu wa Israel nchini Marekani, amesema haifahamu mipango yoyote inayoendelea.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameitaka Israel kuchangia hatua zitakazotuliza mzozo katika kanda hiyo ya Mashariki ya Kati licha ya shambulizi la Iran dhidi yake. Kansela Scholz amewaambia waandishi wa habari mjini Shanghai nchini China kwamba vilevile Iran lazima iache uchokozi.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, David Cameron amekiambia kituo cha Utangazaji cha BBC kwamba kwamba Uingereza haiungi mkono ulipizaji kisasi.

Baadhi ya serikali za Afrika nazo zimezihimiza Israel na Iran kuepusha kuchochea mgogoro zaidi.