ACT Wazalendo kuadhimisha miaka 10 ya kuanzishwa, kufanya shughuli za kijamii

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:09 PM Apr 15 2024
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo.
Picha: Elizabeth Zaya
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kinatarajia kuadhimisha miaka 10 ya kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo za kisiasa, kijamii na kutoa misaada ya kibinadamu kwa wagonjwa katika hospitali mbalimbali nchini na waathirika wa mafuriko.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo, amesema kilele cha maadhimisho hayo ni Mei 5 mwaka huu lakini kabla yah apo watakuwa wanafanya shughuli mbalimbali kuanzia mwezi huu.

Shangwe amesema mambo mengine ambayo wanatarajia kufanya katika kuadhimisha miaka 10 ya chama hicho kufanya kongamano la vijana ambalo linatarajiwa kufanyika Zanzibar April 21 mwaka huu likilenga kujadili dhima na wajibu wa kundi hilo katika kupigania Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Pia, amesema wanatarajia kufanya mkutano wa kidemokrasia Moshi mkoani Kilimanjaro Aprili 27 mwaka huu na kuzindua nembo na bendera mpya.

"Pamoja na ushiriki huu wa mikutano na makongamano, wanachana watashiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kuchangia damu, kufanya usafi kwenye hospitali na kuwafariji wagonjwa,"amesema Shangwe.

"Mkesha wa ACT-Wazalendo utakuwa Mei 4 mwaka huu Makao Makuu Dar es Salaam na na Ofisi Kuu ya chama Zanzibar, mkesha huu utashuhudia kupandishwa kwa bendera mpya za chama na Mei 5 itakuwa ni kilele na sherehe za maadhimisho haya na  zitafanyika mkoani Kigoma na Mwenyekiti wa chama, Othman Masoud Othman, atahutubia taifa."