CAG abaini ‘madudu’ ofisi za balozi Tanzania

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:37 PM Apr 16 2024
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),  Kichere.
PICHA: MAKTABA
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kichere.

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23, imebaini ‘madudu’ katika ofisi za Balozi za Tanzania kwenye nchi mbalimbali ikiwamo gharama kubwa za kodi ya pango ya Sh. bilioni 18.46 kwa majengo ya ofisi na makazi kwenye balozi 39 za Tanzania nje ya nchi.

Katika ripoti hiyo inaonesha ukarabati wa jengo la ofisi ya Balozi Kampala, Uganda haujaanza licha ya kuwa na bakaa ya fedha Sh. bilioni 1.78 tangu mwaka 2018.

Pia, inaonesha gharama za ukarabati wa jengo la zamani la ubalozi wa Tanzania, lililoko Washington ulikuwa na dosari ambapo gharama ya mkataba iliyonukuliwa ilizidi gharama iliyokadiriwa na mshauri elekezi kwa asilimia 94, ukarabati haukujumuishwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka.

Aidha, amesema kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani cha asilimia 20 kilichotajwa katika mchanganuo wa gharama za kazi na ambacho kililipwa katika malipo ya awali hakikuwa na uhalisia kwa kuzingatia kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani ya Washington ambayo ni asilimia sita.

CAG amebaini kulikuwa na hatari ya kulipa riba kwa mkandarasi kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya hati za madai (IPCs) Na. 1 na 2 ambazo zilitolewa tarehe 15 Machi 2023 na 05 Mei 2023, mtawalia, na hazijalipwa mpaka sasa. Mkandarasi alikuwa anawasiliana moja kwa moja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pasipo kumtumia Meneja Mradi.

MADUDU UNUNUZI

Amesema taasisi 25 zilibainika hazikutekeleza mipango yake ya ununuzi yenye thamani ya Sh. bilioni 565.49, mamlaka nne za maji zilifanya ununuzi wa jumla ya Sh. milioni 537.93 bila kuwa na mipango ya ununuzi ya mwaka; na taasisi sita zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 1.82 bila kujumuishwa katika mipango yao ya ununuzi ya mwaka.

CAG amebaini miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 635.12 ilianza bila kuwa na cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira na kijamii, wakati ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 7.12 kwa taasisi 15 ulifanyika bila kuidhinishwa na bodi za zabuni.

Pia amebaini upungufu kwenye michakato ya utoaji wa zabuni, ambapo taasisi 16 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 149.56 bila kutumia mfumo wa kielekitroniki.

Kadhalika, amesema taasisi sita zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 77.67 bila kutumia njia za ushindani wa bei. Ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 2.16 ulifanyika bila kutumia mikataba na mikataba yenye thamani ya Sh. bilioni 4.78 haikupekuliwa na Wanasheria.

Amebaini upungufu katika kutimiza majukumu ya kimkataba ambapo taasisi 11 zilichelewa kulipa madai ya Sh. bilioni 38.73 na kutolipa madai ya Sh. bilioni 19.37 ndani ya muda uliokubaliwa.

Wizara ya ujenzi haijalipa riba ya Sh. bilioni 17.48 iliyotokana na uamuzi wa usuluhishi uliofikiwa tangu mwaka 2014, pamoja na riba ya Sh. bilioni 34.82 iliyotozwa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuchelewa kulipa wakandarasi.

Pia, mikataba 46 ya ujenzi ilikosa dhamana za utendaji kazi zenye thamani ya Sh. bilioni 383.76.

Hata hivyo, amebaini Tume ya Madini na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) hazikudai dhamana ya utendaji kazi na malipo ya awali yenye thamani ya jumla Sh. milioni 675.90 kwenye mikataba iliyositishwa.

Amebaini miradi iliyotelekezwa yenye thamani ya Sh. bilioni 7.12 na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 200.01.