Dereva aliyesababisha vifo vya wanafunzi 8 afikishwa mahakamani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:37 PM Apr 17 2024
Ajali ya basi la wanafunzi lililosombwa na maji Arusha.
PICHA: MAKTABA
Ajali ya basi la wanafunzi lililosombwa na maji Arusha.

DEREVA aliyekuwa akiendesha basi la shule ya Ghati Memorial, Luqman Juma, lililopata ajali na kuua wanafunzi wanane Aprili 12, 2024, amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha na kusomewa mashtaka nane ya kuua bila kukusudia.

Wakisoma mashtaka hayo, Waendesha mashtaka wa serikali Yunis Makala na Amina Kiango wamesema mshtakiwa huyo akiwa dereva akiendesha gari T496EFK Toyota hiace Aprili 12, mwaka huu bila kuchukua tahadhari na kuzingatia usalama wa abiria aliowabeba waliokuwa chini ya uangalizi wake, aliliendesha gari hilo kwenye maji ya mvua eneo la Engosengiu, Sinoni na kushindwa kulimudu hadi kupelekea kusombwa na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane wenye umri wa miaka kati ya mitatu na kumi na tatu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mshatakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo ya Wilaya ya Arusha haina mamlaka ya kusikiliza shauri lake ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi Sheila Manento aliahirisha kesi hadi Aprili 30, 2024 itakapokuja kutajwa tena.