Kinana akemea ukabila Rorya

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:50 PM Apr 15 2024
news
Picha: Maulid Mmbaga
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuachana na tabia za ukabila akieleza kuwa ni mambo ya kizamani na yanawagawa.

Akizungumza leo na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, amesema nchi kuwa na makabila ni jambo la kawaida lakini ukabila ni jambo baya, akieleza kuwa kumuhukumu mtu kwa jambo ambalo hana uwezo nalo sio sahihi.

Kinana amesema hayo baada ya baadhi ya wajumbe kuibua hoja kwamba kuna mambo yanafanyika wilayani hapo ambayo yanaashiria kuwepo kwa changamoto ya ukabila miongoni mwao.

Amesema Baba wa Taifa Julius Nyerere ametoka mkoa huo, na ni kabila dogo sana lakini ameongoza nchi kwa miaka 24, na kwamba alipendwa, aliheshimiwa, alithaminiwa na alitukuzwa sio kwa sababu ya ukabila bali ni kazi aliyokuwa anafanya, utendaji na uadilifu wake uliomfanya aheshimika Tanzania, Afrika na duniani.

"Sasa usimpe mtu nafasi ya uongozi kwasababu ya kabila lake, dini au umbile usimhukumu, hayo ni mambo ya kizamani sana, tuangalie mtu anauwezo atafanya kazi atajituma na kujitolea, mnampima kwa vigezo sio kwamba huyu ni ndugu yangu.

"Mtu mmoja kwenye kabila lako akipata cheo anakusaidia nini hasa wewe mwenyewe? Uko kijijini kule mngekuwa mnagawana mshahara sawa, kila mmoja anakuletea 300,000 kutoka kwenye mshahara wake kwasababu ni kabila lako sawa... wekeni watu kwa uwezo," amesisitiza Kinana.

Aidha, ameeleza kuwa jambo ambalo Baba wa taifa aliwaachia ni umoja wa kitaifa, akitolea mfano kwamba kuna nchi jirani,  hakuzibainisha kwa majina, kwamba mtu hawezi kuwa gavana wa jimbo kama anatoka sehemu nyingine, lakini Tanzania wanafanya kazi nchi nzima.