Kinana ataka utaratibu mzuri wa ukosoaji

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:23 PM Apr 16 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.
Picha: Mauld Mbagga
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimekemea kitendo cha baadhi ya viongozi wa chama hicho kuwadhalilisha watendaji wa halmashauri hadharani akieleza kuwa kama wanajambo waende kuwaeleza madiwani, mwenyekiti wa halmashauri, mkuu wa wilaya na mbunge, kwakuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni za utumishi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, ndiye aliyetoa kauli hiyo Leo wakati akizungumza katika kikao cha ndani na Wajumbe wa Kamati Kuu za Siasa za chama hicho, Wilayani Bunda, mkoani Mara, amesema wakurugenzi hawa wanafanya kazi nzuri na  wanapolaumiwa wanabaki kusononeka kwasababu hawana pa kusemea.

Amesema wakurugenzi hao wanastahili kupewa heshima zao kama binadamu na watumishi kulingana na kazi wanazofanya  na inapobainika wamekosea hawapaswi kuparamiwa  kwenye mikutano ya hadhara bali mifumo yakiutumishi inapaswa kuzingatiwa katika kuwawajibisha na si utaratibu unaotumika wa kuwasema hadharani.

"Usisimame kwenye mkutano wa hadhara ukaanza kumdhalilisha mtendaji wa serikali ambae ni sehemu ya serikali ya chama cha mapinduzi, kwa jambo ambalo wakati mwingine hata ushahidi huna, au unakuta ni uzushi umeambiwa. Serikali inautaratibu wake nyia ya mawasiliano kati ya chama na halmashauri ni kupitia kwa wenyeviti na wakuu wa wilaya.

"Mnapokwenda kukagua miradi musianze tena kutoa kauli za kukashifu watu, ukiona kuna mapungufu mahali, muulize mkuu wa wilaya au mwenyekiti wa halmashauri wao watamtafuta mkurugenzi watazungumza nae, lakini ukiitaja halmashauri wakati kuna serikali watakosa nguvu ya kufanya kazi, nawasihi tuache tabia hiyo wote tunakosea," amesema Kinana