Kinana,mawaziri kujadili mgogoro mpaka wa Sirari

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:27 PM Apr 15 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana
Picha: Maulid
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana amesema ataenda kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Mchemba na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata kujadiliana ili kupata ufumbuzi wa adha zinazowakuta Wananchi kwenye mpaka wa Sirari.

Mpaka huo unaounganisha Tanzania na Kenya unalalamikiwa na baadhi ya Wananchi kutokana na changamoto ya kuvusha bidhaa na wakati mwingine hata wakiruhusiwa  wamekuwa wakitozwa gharama kubwa ikilinganishwa na thamani ya mzigo waliobeba hali inayowaongezea  ugumu wa maisha.

Akizungumza leo katika mkutano wa ndani uliofanyika Tarime Mjini, Kinana amesema hakuna haja ya kuwatesa wananchi kama wanapata bidhaa kwa gharama nafuu.

"Hili ni jambo inabidi nikakae na Waziri wa Fedha na Kamshina wa Mamlaka ya Mapato ili tuelewane na maagizo yatolewe. Kwa sababu mnaweza kuwa na sera nzuri na msimamo alafu watu walioko pale wakawa hawafuati sheria," amesema 

Akizungumzia changamoto hiyo, Mbunge wa Tarime Mwita Waitara amesema kinachofanyika katika mpaka huo bidhaa zinazopatikana Kenya gharama yake ni nafuu ikilinganishwa na Tanzania.

"Saruji ukiitaka ya Kenya na inakuja hadi nyumbani kwako unaipata kwa Sh 15,000 hadi Sh 17,000 lakini hapa Tanzania Sh 25,000 kwahiyo kama mwananchi wa kawaida lazima atatafuta nafuu.

"Kama mkulima Kenya unapata kwa Sh 50,000 hadi Sh 60,000 hapa Tanzania inaenda hadi Sh 100,000 kuangalia mtu wakijijini tofauti ya Sh 20,000 ni hela nyingi," amesema Waitara

Amesema wananchi wanachokifanya mpakani wameweka utaratibu wanazofanya biashara za jumla wanaruhusiwa kuingiza bidhaa hizo kwa kwasababu wamepewa vibali na wanalipa kodi.

"Mwananchi akipitisha bidhaa anakamatwa anaambiwa amepitisha kimagendo na bodaboda wanakamatwa na pikipiki zao kutaifishwa na kupigwa faini," amesema 

Waitara amesema kutokana na urasimu huo umekuwa chanzo cha vitendo vya rushwa kuendelea mpakani hapo kwa kuelewana na maaskari wapitishe kwa gharama nafuu kwa kufanya mazungumzo ya kificho.

"Tulichoomba Sisi na nilishapeleka Bungeni waweke utaratibu bidhaa ndogondogo ndogondogo watu walipe kodi ya kawaida ili wapate huduma,lakini kuweka gharama na masharti magumu watu wanaingia uchochoroni na yanakuwa mapambano serikali inakosa kodi na kuna kuwa na mahusiano mbaya kati ya serikali na wananchi wake," amesema Waitara

Mmoja wa Wananchi Charles Mtatiro ambaye pikipiki yake ilitaifishwa baada ya kukamatwa akivusha mifuko miwili ya sukari kutoka Kenya huku akisema  wanapitia wakati mugumu.

"Hatuoni tija ya kuishi katika mpaka huu,Mimi kazi yangu bodaboda walinikamata na wakataifisha pikipiki yangu kila nilipojaribu kufuatilia hawakuwa na habari na Mimi tunakiomba chama kiiagize serikali yake jambo hili hatulipendi na halina haki kwetu," amesema