Mamilioni Mfuko wa Wanawake hayajarejeshwa kwa miaka 20

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:28 AM Apr 16 2024
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), charles kichere.
PICHA: MAKTABA
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), charles kichere.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini Sh. milioni 664.50 hazijarejeshwa kwa muda wa miaka saba hadi 20 kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.

Pia amebaini kampuni ya ulinzi ya Suma JKT na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hawajakusanya jumla ya Sh. bilioni 1.86 walizopaswa kukusanya.

Vilevile, vituo vinne vya ukaguzi wa afya katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege vilishindwa kukusanya tozo za ukaguzi Sh. milioni 879.11 baada ya ukaguzi huku Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi (PHAB) ikishindwa kukusanya Sh. milioni 768 kutoka kwenye vituo vya afya 2,640 vilivyosajiliwa upya.

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa mwaka 2022/23 iliyowasilishwa bungeni jijini hapa jana, CAG Charles Kichere anabainisha kuwa Mfuko wa Wanawake ulitoa mikopo ya Sh. bilioni 1.13 kwa vikundi vya wanawake na watu binafsi bila kuikatia bima na kati yake, mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 664.5 haijarejeshwa.

BIL 32/- ARDHI

CAG anasema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia imeshindwa kukusanya Sh. bilioni 32.43 zilizotolewa kwa halmashauri ili kutekeleza mipango ya upimaji na umilikishwaji hati miliki za ardhi baada ya kumalizika kwa muda wa urejeshwaji fedha hizo Juni 30, 2022.

Katika hospitali za rufani, CAG amebaini kuwa hospitali nne zilishindwa kukusanya Sh. milioni 452 kwa kushindwa kufuatilia fedha za matibabu ya wagonjwa wanaotumia bima za mifuko mingine, wakati Sh. milioni 111.76 hazikukusanywa baada ya hospitali tatu za rufani kutoa misamaha ya gharama za matibabu kwa wagonjwa wasio na sifa za kupata misamaha ya matibabu.

Pia amebaini Sh. bilioni 61.09 hazikukusanywa na taasisi 29 licha ya kutoa huduma. Fedha hizo zimeripotiwa kama madai huku Sh. bilioni 4.058 katika akaunti za taasisi tano za serikali zikikaa muda mrefu bila kutumiwa na Sh. bilioni 7.73 zilikusanywa na taasisi tatu nje ya mifumo ya ukusanyaji.

MKATABA TATA

Vilevile, CAG amebaini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) iliingia makubaliano ya upangishaji eneo la ardhi lenye mita za mraba 11,000 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam kwa shughuli za kibiashara kwa masharti nafuu yanayopelekea ukusanywaji mdogo wa mapato ya serikali, malipo ya pango kwa mita mraba yalikuwa Dola za Marekani 4.36 tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2018, ambayo yalipunguzwa hadi dola za Marekani 4.09 kwa mita mraba.

UKIUKWAJI KANUNI

CAG pia amebaini taasisi saba zimekiuka kanuni za fedha kwa kuwa na bakaa ya Sh. bilioni 2.45 katika akaunti zao za matumizi za masurufu huku 13 zikifanya malipo ya Sh. bilioni 2.87 bila kudai stakabadhi za kielekitroniki kutoka kwa wauzaji bidhaa na watoa huduma.

Pia ukarabati wa jengo la ofisi ya Balozi Kampala, Uganda haujaanza licha ya kuwa na bakaa ya Sh. bilioni 1.78 tangu mwaka 2018 na kumekuwa na gharama kubwa za kodi ya pango ya Sh. bilioni 18.46 kwa majengo ya ofisi na makazi katika balozi 39 za Tanzania nje ya nchi kwa mwaka wa fedha 2022/23.

DOSARI MSD

CAG pia amebaini Bohari ya Dawa (MSD) ilinunua mashine 10 za kuondoa maumivu, ukakamavu na mkazo wa misuli kwa bei ya Sh. milioni 136.7 na kuacha kununua vifaa hivyo kwa mzabuni aliyebainika kuwa na bei ndogo wakati wa ushindani ya Sh. milioni 103.2, hivyo kusababisha gharama za ziada ambazo zingeepukika za Sh. milioni 33.5.

Mdhibiti amebaini ununuzi wa vifaatiba kwa wazabuni 32 waliopewa zabuni zenye thamani ya Sh. bilioni 4.14 bila kufanyiwa uchambuzi wa awali na kuidhinishwa na bodi ya zabuni.

Pia amebaini vifaatiba vyenye thamani ya Sh. bilioni 13.37 ambavyo ununuzi wake haukuwa umeanza. Amebaini uchelewaji ununuzi na usambazaji vifaatiba katika vituo vya afya kwa siku zinazoanzia 23 hadi 1,458 tangu fedha zilipopokewa na bohari hadi vifaatiba vilipofika kwenye vituo vya afya, vituo 21 vya afya vilipokea vifaa vyenye thamani ya Sh. bilioni 1.68 ambavyo vilikuwa havijaanza kutumika.