Mbunge ataka Tume Huru Uchaguzi Zanzibar

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:57 AM Apr 16 2024
Mbunge wa Jimbo la Konde (ACT-Wazalendo), Mohammed Said Issa.
PICHA: MAKTABA
Mbunge wa Jimbo la Konde (ACT-Wazalendo), Mohammed Said Issa.

MBUNGE wa Jimbo la Konde (ACT-Wazalendo), Mohammed Said Issa, ameitaka serikali kuifanyia mabadiliko Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kama ilivyofanyika kwa Tume ya Uchaguzi Tanzania ili kuondoa udanganyifu unaofanyika visiwani humo wakati wa uchaguzi.

MBUNGE wa Jimbo la Konde (ACT-Wazalendo), Mohammed Said Issa, ameitaka serikali kuifanyia mabadiliko Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kama ilivyofanyika kwa Tume ya Uchaguzi Tanzania ili kuondoa udanganyifu unaofanyika visiwani humo wakati wa uchaguzi.

Mbunge huyo amesema licha ya serikali kufanyia marekebisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuibadili kuwa Tume Huru ya Uchaguzi bado kwa upande wa Zanzibar inatambulika kama Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kudai kuwa hakuna kilichobadilika kwa upande huo.

Amesema ili uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu ufanyike kwa uhuru na haki, ipo haja ya serikali kubadili Tume hiyo ili nayo iwe huru na kufanya kazi chini ya sheria mpya iliyopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Bunge hili limepitisha na Rais tayari ametia saini na ni sheria tayari licha ya kuwa sheria hii inatumika kama ya Tanzania ila huku Zanzibar bado wakala anayetumika ni yuleyule inatakiwa naye afanyiwe marekebisho ili yasijitokeze tena yale ya uchaguzi uliopita,” amesisitiza.

Kuhusu uwajibikaji wa Tume hiyo, aliitaka kuwajibika ipasavyo ili kuondoa udanganyifu alioutaja kutokea katika uchaguzi wa marudio wa madiwani katika maeneo mbalimbali nchini akiutaja kutokuwa huru.

SERIKALI KUNUNUA MAHINDI

Wakati huo huo, serikali imewataka wakulima wote nchini pamoja na wafanyabiashara kuacha kuuza mazao kwa bei ya hasara ndani na nje ya nchi na kuwa ipo tayari kununua mazao hayo kwa bei elekezi ili kuacha kuwaumiza wakulima.

Kauli hiyo imetolewa jana bungeni na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2024/25 na kueleza kuwa kwa sasa serikali imeruhusu kuuza mazao kwa nchi jirani, lakini sio kwa bei inayomuumiza mkulima,

Aidha, amewataka wakulima wa mahindi ambao tayari wameaanza kuvuna kutokukimbilia kuuza mahindi yao kwa bei rahisi kwa kuwa serikali inakaribia kuanza kununua na wafanyabiashara wote wana maelekezo namna ya kuuza mahindi katika nchi zenye uhitaji mkubwa.

“Tunawaruhusu wauze kwa nchi jirani zenye matatizo ya chakula,lakini hatutawaruhusu kuuza mahindi kwa bei ya kutupwa kwani atakayepata hasara ni mkulima kwahiyo tumewaelekeza haya na tayari tumeanza kuwapa vibali vya usafirishaji nje. Tumekubaliana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na tuwauzia unga badala ya mahindi na tumeanza kusaga jumla ya tani 30,000 hivyo tuwaondoe hofu juu ya mavuno makubwa mtakayokuwa nayo,” amesema.