Mpango aiagiza Wizara Ardhi kulinda bustani za kijani

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:33 AM Apr 16 2024
MAKAMU wa Rais, Dk. Phillip Mpango.
PICHA: MAKTABA
MAKAMU wa Rais, Dk. Phillip Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk. Phillip Mpango, ameiagiza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuchukua hatua za kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kijani ili yasiharibiwe au kubadilishwa matumizi.

Dk. Mpango amesema hayo jijini hapa, alipokuwa akifungua Kongamano la Jukwaa la Maendeleo Endelevu, kuhamasisha uwekezaji katika bustani za kijani kwa maendeleo endelevu.

Amesema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa, zinapaswa kuchukua hatua za kulinda maeneo yote yaliyotengwa nchini kwa ajili ya bustani za kijani.

Amesema, kutokana na changamoto zilizopo maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya bustani za kijani katika miji na majiji nchini yameharibiwa na mengine kubadilishwa matumizi kinyume na mipango miji.

"Pia mamlaka za serikali za mitaa zihakikishe kuwa zinatunga sheria ndogondogo ambazo zitatumika kulinda maeneo haya ili yasiharibiwe wala kubadilishwa matumizi yake," amesema.

Ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuanzisha tuzo maalum ya kushindanisha bustani bora za miji na majiji.

Kadhalika, ameuagiza mkoa wa Dodoma kabla ya mwisho wa mwaka huu kuwa na bustani tatu za kijani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 56 ya Watanzania wanaishi mjini na kama hatua hazitachukuliwa hali itazidi kuwa ngumu.