Musukuma: Makali kikokotoo yanazalisha watumishi wezi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:31 PM Apr 18 2024
MBUNGE wa Jimbo la Geita (CCM), Joseph Kasheku.
PICHA: MAKTABA
MBUNGE wa Jimbo la Geita (CCM), Joseph Kasheku.

MBUNGE wa Jimbo la Geita (CCM), Joseph Kasheku (Musukuma), ameitaka serikali kuchukua hatua za dharura kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu ili kuepusha kuongezeka kwa watumishi wezi katika taasisi mbalimbali wanaotaka kujikwamua baada ya kustaafu.

Msukuma alitoa kauli hiyo bungeni wakati akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa mwaka 2024/25.

Amesema ni wakati wa serikali kuliona suala hilo kama sehemu ya dharura kwa kuwa kila mkutano wa viongozi wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), limekuwa likiibuka na kushauri kurejesha kanuni ya awali ya asilimia 50.

“Kwa uelewa wangu mimi kama daktari wa akili, ninaona ni kama tunaenda kutengeneza taifa la watumishi wezi kwa sababu wanalalamika sana kuhusu suala la kikokotoo, kwa hali hii mstaafu anapewa kiasi kidogo cha fedha ambacho hakimtoshi hata kuanza maisha kwa hali hiyo lazima aibe kwasababu anajua hela zake hatopewa,” amesema Musukuma.

“Juzi nilimsikia Katibu Mkuu wa CCM, Emamnuel Nchimbi akisema suala hilo haliwezi kuwa kilio cha kila siku na serikali inaendelea kuweka pamba masikioni (haisikii),” amenukuu. 

Aidha, amewataka mawaziri husika na serikali kukaa pamoja na kuona namna ya kurejesha kanuni ile ya awali ya asilimia 50 ili kuondoa vilio vya watumishi ambavyo alivitaja kudumu kwa muda mrefu.

“Kama kuna tatizo tuambieni maana hawa watumishi ni wetu, vinginevyo hakuna mtumishi atakuwa mwaminifu kwani unakuta amebakiza miaka mitatu ana watoto wamemaliza chuo kikuu na anatakiwa astaafu akajitegemee.”

“Mtumishi huyo hana nyumba yupo nyumba ya serikali na anategemea kuondoka na asilimia 33 huyo lazima abebe mzigo aondoke nao,” amesisitiza Msukuma.

Mbunge wa Jimbo la Chemba (CCM), Mohamed Monni, ameliomba Bunge kushughulikia suala hilo kama ilivyo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ili hali iwe salama.

“Kule nje inaonekana ni jambo ambalo hatuliongelei kabisa hivyo kwanini tuendelee kuishi na watu wenye manung’uniko makubwa wakati wanatusaidia kazi zetu,” amesema.

Mbunge wa Iltilima (CCM), Njalu Silanga, ameshauri Bunge lirudi mezani na kufanya utafiti wa kutosha kuhusu suala hilo ili kuona njia bora ya kuwasaidia wastaafu na kuendana na matarajio yao tofauti na sasa.

“Wazo la kuhamisha kikokotoo cha asilimia 50 kwa 50 kupeleka asilimia 67 kwa 33 lilikuwa ni jema, lakini hatukufanya utafiti vizuri ili kuendana na matarajio ya wastaafu kwani wamejiwekea kuwa wakistaafu atapata asilimia 50 ya Sh. milioni 100, lakini matokeo yake anaambiwa atapata asilimia 33 tayari hiyo ni shida,” amesema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi akiwa mkoani Rukwa katika ziara yake ya mikoa sita aliahidi kufikisha hoja ya kikokotoo kwa Rais Samia kwaajili ya utatuzi, akisisitiza kuwa imekuwa kero kubwa kwa wastaafu.

Jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliambia Bunge kuwa serikali imepokea maoni ya wabunge na wadau mbalimbali kuhusu kikokotoo na kwamba litaendelea kufanyiwa kazi.