Dk. Mwinyi: Kero za muungano zinatafutiwa dawa

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 03:09 PM Apr 15 2024
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
PICHA: IKULU
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.

Ameyasema hayo kwenye viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi, nje ya mji wa Zanzibar wakati wa uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema kwa nyakati mbalimbali juhudi zikichukuliwa na serikali zote mbili ambazo ni pamoja na kuundwa kwa tume na kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja za Muungano na miongoni mwa tume na kamati hizo ni Kamati  ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushughulikia masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.

Amesema kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokewa na kujadiliwa na kati ya hoja hizo, 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Amesema, hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi na imani yake kuwa, kwa utashi na dhamira ya dhati ya serikali za pande zote mbili, zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.

Aidha, amesema katika kipindi cha 2021 hadi 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwapo na utatuzi wa changamoto za Muungano, umeongeza imani ya Watanzania kwa serikali na hivyo kuimarisha, kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu wa Tanzania ambao ni tunu muhimu na fahari ya nchi.

“Nawahakikishia wananchi wote wa Tanzania, kwamba serikali zote mbili zitaendelea kuchukua hatua ili nchi yetu iendelee kupiga hatua za maendeleo na ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu.”

Amesema wananchi wa Tanzania wana matumaini makubwa na Muungano huo, pamoja na taasisi zote zinazohusika katika kuufanya uendelee kudumu na kuimarika na kwamba ni vyema kutafakari kwa kina historia yake, dhamira ya waasisi wake na manufaa yake.

Kadhalika, Watanzania wanaposherehekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, wana wajibu wa kujipongeza kwa mafanikio makubwa ambayo nchi imeyafikia katika nyanja zote za maendeleo kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.

“Katika kipindi hiki cha miaka 60, Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote. Muungano wetu umeipa heshima kubwa nchi yetu katika Jumuiya ya Kimataifa,” amesema Dk. Mwinyi.

Amesema hiyo imetokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano iliyoasisiwa na viongozi ambao ni Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano.

Aidha, dhamira yao ya dhati na maono ya waasisi hao, kumewezesha kupata hatua kubwa ya mafanikio yaliyofikiwa katika kudumisha na kuimarisha Muungano wa Tanzania.

“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu katika shughuli mbali mbali unaongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu,” amesema.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewashukuru Rais Dk. Mwinyi na Dk. Samia, wanavyoliongoza taifa kwa misingi ya kusimamia Muungano.

Amesema, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya Muungano na Mazingira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinawajibu wa kuielewesha jamii juu ya historia ya Muungano kwa vizazi vilivyopo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk. Selemani Saidi Jafo, amesema historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeundwa na sababu nyingi hadi kufikia kusainiwa kwa hati ya Muungano mwaka 1964 chini ya waasisi wake Hayati baba wa Taifa Julius Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Akitaja baadhi ya sababu hizo zikiwemo urafiki na udugu wa damu wa wananchi wa pande mbili za Muungano, lugha ya Kiswahili iliyowaunganisha watu wa pande hizo, pamoja vyama vya ukombozi vya TANU na ASSP, Waziri Jafo alisema vilitoa mchango mkubwa kwenye Muungano huo.

Amesema katika kusherehekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wanatarajia kuzindua kitabu maalum kinachoeleza historia ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufundishiwa shule za sekondari nchi nzima.

Uzinduzi wa sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na ufunguzi wa Maonesho maalum ya Taasisi za Muungano chini ya kaulimbiu, “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, unaashiria kuanza rasmi kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo upandaji wa miti, usafi wa mazingira na ushiriki wa wananchi na viongozi kwenye matukio ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi kwa maeneo mbalimbali ya Tanzania.