Serikali yapeleka msaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:15 PM Apr 15 2024
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, akikagua tani 300 za chakula zilizotolewa na serikali.
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, akikagua tani 300 za chakula zilizotolewa na serikali.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa tani 300 za chakula Kwa waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Akikabithi msaada huo Kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, amesema Rais ametoa msaada huo kusaidia waathirika wa mafuriko katika wilaya hiyo.

Kunenge amesema wamekuwa wakipokea misaada ya waathirika kutoka serikalini na sasa wamepokea   binafsi kutoka kwa Rais binafsi kiasi tani 300 na watazigawa kwa wote waliolengwa kama ilivyoelekezwa.

Pia amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa kwa mchango wake wa kuendelea kutafuta wafadhili wa kusaidia waathirika wa mafuriko hayo na kwamba watahakikisha misaada yote inayotolewa inawafikia.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, amemshukuru Rais Kwa namna alivyoguswa na changamoto ya wananchi wa Rufiji walioipata na kutoa misaada hiyo.

Akikabithi msaada huo kwa niaba ya Rais Samia, Innocent Mbilinyi, amesema ameleta msaada huo binafsi kutoka kwa Rais ili kisaidia waathirika hao waweze kupata chakula na mahitaji mengine muhimu.