TAMISEMI yataja vipaumbele vya bajeti yake

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:23 AM Apr 17 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa.

WIZARA ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeweka sura ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi 2024/25 ya Sh. trilioni 10.125 na kutoa vipaumbele katika Elimu, Afya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

ELIMU

Imepanga kutumia Sh. trilioni 1.02 kupitia ruzuku ya Serikali Kuu na washirika wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli katika sekta ya elimu katika usimamizi, uendeshaji wa elimu msingi na sekondari.

Mchengerwa ametaja shughuli zitakazotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, umaliziaji wa mabwalo 362 kati ya hayo 15 ni msingi na 347 ni ya sekondari na umaliziaji mabweni 36 kwenye shule za awali na msingi.

Pia, ametaja ujenzi wa shule mpya 184, nyumba za walimu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwenye shule za awali tatu, msingi 400 na sekondari 500.

Ametaja ununuzi wa kemikali za maabara katika shule mpya 234, utoaji wa ruzuku ya elimu bila ada kwa shule za msingi 17,986 na sekondari 4,894; ununuzi na usambazaji wa vitabu 2,215,877 kwa shule za msingi na 11,880,828 kwa shule za sekondari pamoja na vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na kujifunzia elimu ya awali kwenye shule 4,500 pamoja na ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari.

Kadhalika, kutoa mafunzo ya maadili kwa wakuu wa shule 17,220, viongozi na watumishi wa TSC 460 katika ngazi ya wizara na wilaya, kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwenye shule za awali na msingi kwenye halmashauri 140, kutekeleza mpango wa shule salama kwenye shule za awali na msingi 2,500.

Aidha, amesema serikali itaanzisha madarasa janja 10 kwa ajili ya ufundishaji mubashara katika halmashauri 10 yatakayosaidia kupunguza tatizo la uhaba wa walimu hususani katika masomo ya hesabu na sayansi.

MIUNDOMBINU

Katika sekta ya ujenzi amesema serikali inatarajia kutumia Sh. bilioni 841.19 kwaajili ya ujenzi, matengenezo, ukarabati wa miundombinu ya barabara, usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini.

Kati ya fedha hizo Sh. bilioni 257.03 ni za Mfuko wa Barabara, Sh. bilioni 127.50, Mfuko Mkuu wa Serikali, Sh. bilioni 325.77 ni za tozo ya mafuta ya petroli na dizeli ya Sh. 100 kwa lita, Sh. bilioni 4.03 za mapato ya ndani kupitia Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam na Sh. bilioni 126.85 ni fedha za nje.

Katika utekelezaji huo yanatarajiwa kufanyika matengenezo ya barabara za vijijini na mijini zenye urefu wa kilomita 20,745.31, ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 434.50, ujenzi wa barabara za changarawe zenye urefu wa kilomita 13,802.34, ujenzi wa madaraja 160 na ukarabati wa madaraja.

Shughuli nyingine ni ujenzi na matengenezo ya boksi kalavati 586 na vivuko 15, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 141,070.54, ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi, kudhibiti maeneo ya juu ya Mto Msimbazi.

Vilevile, kufanya ujenzi wa masoko, mitaro ya maji ya mvua, stendi za mabasi, maghala ya kuhifadhia mazao na kujenga barabara kiwango cha lami kilomita 147.5, kuondoa vikwazo vya upitikaji barabarani kwenye wilaya 131 na ujenzi wa barabara kiwango cha lami awamu ya pili kilomita 164 kupitia Programu ya Kuongeza Fursa za Kiuchumi na Kijamii Nchini (RISE).

Ametaja ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 250, kupitia mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam awamu ya pili na kati ya hizo kilomita 132 zimefanyiwa usanifu.

DART KUFUMULIWA

Katika kuboresha utendaji kazi Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Serikali kupitia Waziri wa OR-TAMISEMI, Mchengerwa imesema inaendelea kukamilisha Sheria ya Usafiri wa Umma ili kuihuisha DART kuwa Mamlaka.

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Imetenga Sh. bilioni 17.79 kwa ajili ya kuratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.

Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni nane ni kutoka serikali kuu kwa ajili ya uratibu Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Sh. bilioni 9.79 ni mchango wa halmashauri kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo.

AFYA

Wizara hiyo imepanga kutumia Sh. bilioni 357.85 za ruzuku ya fedha za maendeleo za serikali kuu na washirika wa maendeleo kukamilisha hospitali za halmashauri 118, vituo vya afya 10, ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali za halmashauri 136, vituo vya afya 44 na zahanati 386, ujenzi wa miundombinu ya maji na vyoo katika vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri 117.

UTAWALA

Alisema wizara hiyo inatarajia kutumia Sh. bilioni 190.57 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa na wilaya, kuendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa ikiwemo majengo ya utawala, ikulu ndogo, makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na tarafa katika mikoa 26.