TBS yatoa angalizo wanywaji pombe kuzingatia vipimo

By Restuta James ,, Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 09:45 AM Apr 16 2024
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga.
PICHA: MAKTABA
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa angalizo kwa wanywaji pombe nchini kuzingatia vipimo vinavyotakiwa, ili kuepuka madhara ikiwamo magonjwa ya figo.

Limesema limekuwa likifanya udhibiti wa vilevi visivyo na ubora vinavyotoka nje ya nchi na zinazotengenezwa nchini, lakini tatizo ni wanywaji kutofuata maelekezo ya matumizi ya vinywaji hivyo.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Health Direct, kinywaji aina ya wine chenye kilevi cha asilimia 13 mtu anapaswa kunywa mililita 100 (sawa glasi moja), bia yenye kilevi cha asilimia 4.9 (mililita 285, sawa na chupa tatu), pombe kali yenye kilevi cha asilimia 40 (mililita 30, glasi toti moja), pombe zitokanazo na matunda zenye kilevi cha asilimia 4.9 (mililita 285).

Msasalaga amesema kwa sasa kuna matumizi mabaya ya kinywaji cha ‘enegy drink’ na pombe kali, watumiaji wengi wanatumia bila kufuata maelekezo.

“Utakuta mtu anakunywa wakati hajala, mwingine anakunywa kuzidi kiwango kinachotakiwa, mwisho wa siku anaumwa figo halafu anasema ni pombe feki,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, amesema TBS katika utekelezaji wa majukumu, imepata mafaniko mbalimbali ikiwamo kujenga maabara katika mikoa ya kimkakati ambayo ni Dodoma inahudumia mikoa ya Tabora na Singida.

“Shirika linatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Kaskazini (Arusha). Maabara ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Maabara ya Kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara,” amesema Dk. Ngenya.

Ametaja mafanikio mengine ni ununuzi wa mashine za kisasa za maabara kwa kutumia fedha za ndani pamoja na misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Kuhusu mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara, Dk. Ngenya amesema katika kipindi cha miaka mitatu, viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa Pamoja na kushiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara Afrika Mashariki na Afrika.

Amesema serikali kwa kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya Sh. milioni 250 kwa ajili ya kuwahudumia wajasiriamali wadogo bila malipo.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu, leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini. Kati ya leseni hizo, 1,051 zilitolewa bure na kwa wajasiriamali wadogo.

Dk. Ngenya amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, wadau 5,789 kutoka mikoani walipewa mafunzo ya ujasiriamali.

Amesema TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Vilevile, amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa.

Kuhusu ukaguzi wa bidhaa kutoka nje, Dk. Ngenya amesema kwa kipindi cha miaka mitatu shehena 100,851 zilikaguliwa kabla hazijaingizwa nchini, bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini.

Kuhusu usajili wa bidhaa za vyakula na vipodozi, Dk. Ngenya amesema kwa kipindi cha miaka mitatu shehena 100,851 zilikaguliwa kabla hazijaingizwa nchini.

Pia, amesema bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini.