Uhaba wa petroli waitikisa Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 08:45 AM Apr 17 2024
Uhaba wa mafuta ya petroli.
PICHA: MAKTABA
Uhaba wa mafuta ya petroli.

UHABA wa petroli visiwani Zanzibar umesababisha usumbufu kwa baadhi ya wananchi wakiwamo watumiaji wa vyombo vya moto.

Uhaba huo umesababisha vituo vya kuuzia mafuta kufungwa na baadhi ya magari kushindwa kuendelea na safari baada ya kuishiwa na mafuta.

"Tangu jana gari langu limeniishia mafuta nimeiacha hapo hapo katika kituo cha mafuta," amesema Mussa Khamis, mkazi wa mjini hapa wakati akizungumza na Nipashe.

Amesema kama hali hiyo itaendelea ni hatari na shughuli nyingi za kimaendeleo na kiuchumi zitasita.

Amesema pia kuadimika kwa mafuta biashara ya magendo itajitokeza na serikali kukosa mapato.

Mfanyakazi mmoja katika kituo cha kuuzia mafuta kiliopo Kisauni ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa uhaba wa mafuta umetokana na kuchelewa kufika kwa mafuta kutoka Tanzania Bara.

Amesema ni siku ya pili kituoni hapo hawana mafuta ya petroli na wateja wao wanafika na kuondoka.

"Tunaziomba mamlaka husika kurahakisha upatikanaji wa mafuta ili kuondokana na changamoto hii na isijitokeze tena," amesema.

Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishatii Zanzibar (ZURA), imesema kuwa upungufu wa mafuta ubesabishwa na kuchelewa kufika kwa meli ya mafuta Zanzibar kutoka Tanga ilikokwenda kupakia.

Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Omar Yussuf, amesema meli imefanikiwa kufika salama Mtoni Zanzibar usiku wa kuamkia jana na taratibu za kushusha mafuta zinaendelea.

"Mara tu baada ya kukamilika kwa kazi ya ushushaji mafuta mamlaka itahakikisha inafanyika haraka iwezekanavyo na tayari kazi hiyo imeshaanza," amesema.

Mamlaka hiyo imewaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na inafuatilia kwa karibu kuhakikisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini inarejea kama kawaida na wananchi kutokuwa na hofu.

Uhaba huo wa mafuta kwa baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta umeanza kujitokeza tokea Aprili 11, mwaka huu na hadi majira ya saa nane mchana jana huduma hiyo ilikuwa haijarejea kwenye vituo vingi vya kuuzia mafuta.