Ulaji mabilioni wabainika mashirika ya umma

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:35 AM Apr 17 2024
CAG Charles Kichere.
PICHA: MAKTABA
CAG Charles Kichere.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini mashirika ya umma 17 yenye matumizi ya jumla ya Sh. bilioni 72.36 yasiyo na tija.

Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 13 kulinganishwa na mwaka uliopita ambapo kulikuwa na mashirika ya umma 12 yaliyotumia Sh. bilioni 63.77.

CAG Charles Kichere anabainisha hayo katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23 iliyowasilishwa bungeni.

Anasema amebaini mashirika ya umma 11 yenye matumizi yasiyostahili ya Sh. bilioni 4.64, dosari hiyo ikiwa imepungua kwa asilimia 94 kulinganishwa na Sh. bilioni 77.75 kwa mashirika ya umma 21 mwaka uliotangulia.

Anafafanua kuwa kati ya mashirika hayo, manne yaliripotiwa pia mwaka uliotangulia. Hayo ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

CAG anasema TPA ilitumia Sh. bilioni 33.861, TANESCO Sh. bilioni 26.042, Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Sh. bilioni 6.563, DAWASA Sh. bilioni 3.583.

Mengine ni Shirika la Reli Tanzania Sh. bilioni 1.249, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza Sh. milioni 335.65, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Sh. milioni 270.99, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea Sh. milioni 150.09, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida Sh. milioni 39.56,

Pia yamo Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania Sh. milioni 30.11, Kampuni ya Kutengeneza Nguzo za Zege Tanzania Sh. milioni 23.63, Chuo Kikuu cha Ardhi Sh. milioni 22.32, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Sh. milioni 15.79, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga Sh. milioni 11.78 17 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Korogwe Sh. milioni 11.26.

SHIDA TANESCO

CAG pia anasema TANESCO inakabiliwa na tatizo la kuchelewa utatuzi wa migogoro mitatu inayohusiana na tozo za Kampuni ya Songas Sh. bilioni 109.07 ambapo Oktoba 11, 2001, walitia saini mkataba wa ununuzi wa umeme wa miaka 20.

Anasema utekelezaji wa mikataba na mwenendo wa malipo unaonesha kuwapo mizozo endelevu ambayo haijatatuliwa tangu mwaka 2022 na kuwa shirika hilo lililipa malipo hayo yanayofikia Sh. bilioni 67.94.

Vilevile, CAG anasema kampuni ya Songas imeendelea kujumuisha gharama za kuboresha visima vya gesi katika ankara za kila mwezi kuanzia mwezi Agosti 2022 hadi Juni 2023, zenye thamani ya Sh. bilioni 29.34, licha ya tangazo la kukataa tozo hizo lililotolewa na TANESCO mwezi Desemba 2022.

Anasema ankara iliyotolewa Januari 4, 2023, yenye thamani ya Sh. bilioni 23.94 na Dola za Marekani milioni 4.02 kwa mwezi Desemba 2022, iliibua mzozo unaohusiana na deni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) la Sh. bilioni 11.78 ambalo halijalipwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) kutokana na kukosekana nyaraka za kuthibitisha.

CAG anasema kuwa hadi kufikia Desemba 2023, suala hilo halikuwa limetatuliwa. Muda wa miaka 20 wa mkataba wa ununuzi wa umeme unatarajia kuisha mwezi Oktoba 2024 na kuwapo kwa uwezekano wa kuongeza muda.