Vigogo kuwekwa 'kitanzini'

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:32 AM Apr 15 2024
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
PICHA: MAKTABA
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KAMA si leo basi kesho ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka 2022/23 zitawasilishwa bungeni kwa mujibu wa sheria.

Mkutano wa Bunge la Bajeti leo unaingia katika juma la tatu na Ibara ya 143 ya Katiba ya nchi (1977) inaelekeza kuwa Rais baada ya kukabidhiwa ripoti za CAG, anapaswa kuziwasilishe bungeni kupitia wasaidizi wake ndani ya siku saba tangu kuanza kwa mkutano unaofuata wa Bunge (siku za sikukuu na mwishoni mwa wiki hazihesabiki).

Rais Samia Suluhu Hassan alipokea ripoti ya CAG Machi 28, mwaka huu. Mkutano wa Bunge ulianza Aprili 2, 2024, hivyo kutokana na siku za sikukuu na mwisho wa wiki kutohesabika, zimesalia siku mbili kati ya saba kuwasilisha ripoti hizo bungeni kukidhi matakwa ya kikatiba.

Kuwasilishwa ripoti bungeni na hivyo kuwa wazi kwa umma, kunatarajiwa kuwaweka 'kitanzini' baadhi ya watendaji wa serikali ambao CAG Charles Kichere ameweka wazi kwamba taasisi zao zina dosari kiutendaji ikiwamo matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hao ni pamoja na vigogo wa taasisi kama vile Bohari ya Dawa (MSD), Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salama, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na watendaji wa halmashauri.

Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa mfano, CAG Kichere alidokeza katika wasilisho lake kwa Rais Samia Machi 28, mwaka huu kuwa amebaini bado kuna shida ya ulaji wa 'fedha mbichi' (kutumia fedha za makusanyo kabla ya kuziwasilisha Mfuko Mkuu wa Serikali), udhaifu katika ukusanyaji mapato na kutotenga fedha kwa ajili ya makundi maalum. 

Vigogo wengine wanaotarajiwa kuwekwa 'kitanzini' na CAG ni wa mashirika ambayo yanatajwa kujiendesha kwa hasara. Hayo ni pamoja na Shirika la Posta Tanzania, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Mawasiliano (TTCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Uwekezaji ya TANOIL.

Ripoti za CAG zitakazowasilishwa bungeni ni: Ripoti Kuu ya Ukaguzi; Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Kuu; Ukaguzi wa Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa; Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umma; Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo; Ukaguzi wa Mifumo ya Tehama na Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi.

Pia kuna ripoti za ukaguzi wa ufanisi katika maeneo maalum 14, mojawapo ni hali ya utoaji huduma za ugonjwa wa akili nchini.

Baada ya kuwasilishwa bungeni na mawaziri husika, ripoti za CAG zitakabidhiwa kwa kamati za Bunge zenye mamlaka ya kuifanyia uchambuzi.

Pamoja na hayo, juma hili wabunge watapata majibu ya hoja zilizoibuka kwenye mjadala wa Mapitio ya Utekelezaji Bajeti ya Mwaka 2023/24 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2024/25.

Hoja hizo ni pamoja na sakata la kikokotoo cha mafao ya wastaafu, tishio la kufilisika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ugumu wa upatikanaji mikopo ya elimu ya juu na nishati safi ya kupikia vijijini.

Nyingine ni kilio dhidi ya wanyama hatari kwa binadamu, hasa tembo na mamba, kukithiri kwa mikopo kausha damu, matumizi ya shisha, madeni ya askari magereza na utitiri tozo kwenye sekta ya uvuvi.

Baada ya kuhitimishwa mjadala huo, kutawasilishwa hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa Mwaka 2024/25 itakayojadiliwa kwa siku tatu na kufuatiwa na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itakayojadiliwa kwa siku moja.