Wananchi wajitolea kununua mabati kuboresha sekondari yao

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 09:44 PM Apr 16 2024
Boma la maabara ya fizikia linalohitaji ukamilishwaji ambapo  mbunge wa amekabidhi mifuko 100 ya sasruji ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Boma la maabara ya fizikia linalohitaji ukamilishwaji ambapo mbunge wa amekabidhi mifuko 100 ya sasruji ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.

WAKAZI wa vijiji vitatu, Musoma Vijijini mkoani Mara, wamekubaliana kununua mabati 72 kukamilisha miundombinu ya sekondari yao ikiwamo ujenzi wa jengo la maabara ya somo la fizikia.

Vijiji hivyo ni vya Bujaga, Bulinga na Busungu vinavyounda Kata ya Bulinga ambavyo sasa vina mradi wa ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi ambayo ni fizikia, kemia na baiolojia.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo aliyeitisha kikao kujadili maendeleo ya sekondari hiyo, amesema kwa sasa inahitaji mabati 120 ya rangi na kwamba wamekubaliana kuyanunua.

"Tumekubaliana kila kijiji kuchangia mabati 24, kwa vijiji vitatu yatakuwa 72, mimi mbunge nitachangia 24, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma itachangia 24, jumla mabati 120," Profesa Muhongo amesema.

Amefafanua ssekondari hiyo ilianza kutoa elimu mwaka 2016 na kusajiliwa rasmi mwaka mwaka 2019, na kwamba kwa sasa ina maabara mbili za masomo kemia na baiolojia.

"Katika kikao chetu tumekubaliana kwamba, maabara ya fikizia ambayo imejengwa hadi kwenye renta, ikamilishwe kabla ya Agosti 30 mwaka huu, lakini pia michango vifaa vya ujenzi kutoka kwa wana-Bulinga na wadau wengine wa maendeleo inahitajika,"  amesema.

Amefafanua kuwa wanaopenda kuchangia vifaa  hivyo, waviwasilishe kwa mkuu wa Shule ya Sekondari Bulinga, huku akifafanua kuwa michango ya fedha ipelekwe katika akaunti ya Shule ambayo ipo Benki: NMB yenye akaunti namba 30310029434

Baadhi ya wanafunzi wa Bulinga Sekondari wakiwa kwenye kipindi cha mafunzo kwa vitendo ndani ya maabara yao ya kemia.

"Jimbo letu lina mradi wa ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi fizikia, kemia na baiolojia kwenye sekondari zote za kata. wananchi na serikali wanashirikiana katika utekelezaji wa mradi huu," amesema.

Mbunge huyo amesema, jimbo hilo lina sekondari 26 za kata na mbili za binafsi, na kuongeza kuwa kwa sasa wanavijiji wanaendelea na ujenzi wa  sekondari nyingine 10 kwenye baadhi ya vijiji.