Wataka hatua dhidi ya udhalilishaji viongozi wanawake kwenye mitandao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:37 AM Apr 15 2024
Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe.
PICHA: MAKTABA
Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe.

JUMUIYA ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (JUMIKITA) imelaani udhalilishaji wa viongozi wanawake kwenye mitandao ya kijamii huku ikizitaka taasisi za wanawake kupaza sauti kukemea tabia hiyo ambayo inadhalilisha na kuumiza watu.

Imehimiza vyama vya wanawake kama vile Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Umoja wa Wanasiasa Wanawake (WCP-Ulingo), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na wanaharakati binafsi kujitokeza kulaani vitendo hivyo katika kuunganisha nguvu na kusema "hapana" kwa udhalilishaji wanawake.

Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema ili kulinda maadili katika jamii kwa kizazi cha sasa na kijacho, jamii haina budi kujenga msingi mzuri wa kukemea udhalilishaji mitandaoni bila kujali utofauti wa itikadi za kisiasa, dini au kabila la mtu.

“Hivi karibuni kumezuka tabia mpya ya watu badala ya kujadiliana kwa hoja, kutoa mawazo yao au kukosoa serikali kwa mujibu wa katiba yetu, wameanza kutoa matusi mazito kwa Watanzania wenzao, viongozi wao na wakubwa wao katika umri," amesema Matwebe.

Amesema jumuiya hiyo inaomba viongozi wa dini kusimamia maadili kwa waumini wao katika kipindi hiki ambacho maadili yameporomoka katika jamii ili kurejesha jamii katika msingi ya maadili mema na tamaduni za Kitanzania.

Wiki iliyopita, akiwa katika maadhimisho ya kumbukumbu kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amedai anafahamu baadhi ya watu wakiwamo mawaziri ambao wanatuma watu kumtukana Rais Samia Suluhu kwenye mitandao ya kijamii na kuahidi kuwataja leo iwapo wataendelea.

Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo, amesema watajadiliana na viongozi wenzake katika chama hicho na kutoa tamko leo.

“Kwa sasa siwezi kusema kitu, ninawasiliana na bodi na mkurugenzi na leo ni ‘weekend’ (mwisho wa wiki), pengine kesho tunaweza kuona nini tufanye,“ amesema.

Katika akaunti yake ya Facebook, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba jana alionya watu wenye nia ovu ya kuchafua serikali ya Rais Samia hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani na kuahidi kupambana nao.

“Tulijua kuwa kutakuwapo njama za kukuchafua, sana mwaka 2024 na 2025, tunajua kwenye mikakati yao bado watakuja na mengine ya uongo hivihivi, hatutakubali kuyumbishwa, tutapambana na wanaotumwa na wanaowatuma," amesema katika ujumbe wake huo.