Jeshi la Polisi lijitafakari madai ya kumbambikia raia kesi ya ugaidi

Nipashe
Published at 11:00 AM Apr 09 2024
Mkuu wa Jeshi hilo kwa sasa, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura.
Picha:Maktaba
Mkuu wa Jeshi hilo kwa sasa, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura.

KWA muda mrefu, Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa kwa kukiuka maadili na dhima ya majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao, kwa baadhi ya askari na maofisa wake kujihusisha na vitendo vya rushwa, ubambikaji wa kesi dhidi ya wananchi zikiwamo za madai ya ugaidi.

Pia baadhi ya askari na maofisa wa jeshi hilo wamekuwa wakituhumiwa kushiriki katika vitendo vya ujambazi na kupora fedha za watu na hata kuwaua ili kupoteza ushahidi. Hata baadhi ya vidhibiti vya kesi vinavyoshiliwa katika vituo hivyo, vimekuwa vikidaiwa kuharibiwa na askari wasio waaminifu na matokeo yake kuipaka tope taasisi hiyo muhimu. 

Kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi, viongozi wakuu wa serikali mara kwa mara wamekuwa wakifanya mabadiliko ya wakuu wa jeshi hilo na kuwaagiza kutekeleza majukumu yao kwa weledi huku wakisisitiza kupambana na vitendo vinavyolichafua pamoja na kuwachukulia hatua wale wanaoshiriki vitendo hivyo. 

Rais Samia Suluhu Hassan pia amekuwa akisisitiza mara kwa mara juu ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia maadili na weledi. Sambamba na msisitizo wa Rais, Mkuu wa Jeshi hilo kwa sasa, Inspekta Jenerali (IGP) Camilus Wambura, amekuwa akifanya mabadiliko ya makamanda na wakuu wa vitengo kwa lengo la kuimarisha utendaji. 

Katika mikutano kadhaa ya maofisa wakuu na waandamizi wa jeshi hilo, Rais Samia aliweka bayana kwamba jeshi hilo limepoteza imani kwa wananchi kutokana na baadhi ya maofisa na askari kujihusisha na vitendo vya aibu vikiwamo kubambikia kesi raia, kuomba na kupokea rushwa, kupora fedha na mali za raia, kutishia kuwabambikia kesi za ugaidi na vifo vya raia katika mahabusu zinazosababishwa na vipigo kutoka kwa polisi. 

Kuwapo malalamiko hayo na vitendo vya dhahiri, Rais alimwagiza IGP Wambura kuhakikisha anawashughulikia wale wote wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo na kulirejesha jeshi katika ahadi yake na kuwafanya wananchi kuliamini. 

Licha ya maagizo hayo, kumeibuka tena jambo zito la mwananchi kudai kuwa anahofia usalama wa maisha yake baada ya polisi kumtishia kumbambikia kesi ya ugaidi kutokana na kufuatilia mwenendo wa shauri lake katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kwa ajili ya kukata rufani. 

Mwananchi huyo, Bertha Mabula, ambaye ni mfanyabiashara wa kusindika mazao, alifungua shauri lake katika mahakama hiyo dhidi ya Tumsime Tibaijuka ambaye alimkopesha Sh. milioni 295 lakini lilitupiliwa mbali. Lakini wakati anafuatilia hilo, ndipo kukawapo madai ya kundi la polisi waliokuwa wakimfuatilia ili kumkamata kwa madai ya ugaidi. 

Imedaiwa kuwa polisi hao walimvizia eneo la Tinde kutaka kumkamata lakini walishindwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha lakini sasa kuna madai kwamba dereva aliyempeleka Shinyanga, alikamatwa kwa madai ya kumbeba gaidi na kufikishwa kituo cha polisi Kahama kisha kuhojiwa na kuachiwa. 

Mazingira ya kukamatwa kwa dereva na mfanyabiashara kutuhumiwa ugaidi kwa kutaka kulipua jengo la mahakama kuu yanatia ukakasi na kuibua maswali yasiyo na majibu. Kuna uhusiano gani kati ya ugaidi na mtu anayefuatilia haki yake? Inakuwaje polisi wamvizie mfanyabiashara huyo Tinde na baadaye kumkamata dereva kumtuhumu kuwa alibeba magaidi kutoka Kahama hadi Shinyanga na baadaye kuwarudisha?

Suala la ugaidi linapotajwa kwa namna yoyote katika ardhi ya Tanzania, halina budi kufikiriwa kwa kina marefu na mapana hasa katika zama hizi za kujenga Uchumi ulio imara. Jambo hilo linaweza kukwamisha juhudi za serikali kwa kuwa watu kutoka mataifa mengine wanaposikia kuna ugaidi Tanzania, wanaweza kukatisha au kughairi azma zao ya kuwekeza nchini.

Kwa mantiki hiyo, Jeshi la Polisi lijitathmini kuhusu jambo hili ambalo linaonekana kuwa jepesi lakini lina uzito mkubwa kwa mustakabali wa uchumi wa nchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.