Malengo mashindano ya CAF msimu ujao yaende na uhalisia

Nipashe
Published at 04:49 PM Apr 16 2024
Nembo ya CAF.
Picha: CAF
Nembo ya CAF.

BAADA ya timu zake kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwenye misimu minne iliyopita, Tanzania sasa inauhakika wa kuingiza klabu nne katika michuano inayosimamiwa na shirikisho hilo.

Kila mwaka CAF huandaa na kusimamia mashindano yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho.

Msimu huu unaoendelea na uliopita, Tanzania iliwakilishwa na timu nne, mbili zikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine zilipeperusha bendera yake kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Simba na Yanga zote za Dar es Salaam zenyewe zilikuwa zinashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC na Singida zilipeperusha bendera ya Tanzania Bara.

Lakini pia kwa upande wa Zanzibar, KMKMK na JKU pia walishiriki mashindano hayo ya kimataifa.

Msimu wa mwaka jana tulishuhudia kwa mara ya kwanza, Yanga ikitinga hatua ya fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho (ilifungwa na Waarabu wa Algeria- USM Alger), huku Simba ikiishia hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu huu, vigogo hao wa Tanzania wote wameishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikiondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri ikizima tena ndoto za Simba kusonga mbele kwa kuwafunga kwenye mechi zote mbili walizocheza za hatua hiyo.

Ili kufanya vizuri katika mashindano ya ndani au ya kimataifa, timu husika inahitaji uwezekaji wa kweli. Uwekezaji wa kweli ndio husaidia kufikia malengo na si vinginevyo.

Kama timu yako malengo yake ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara au michuano ya Kombe la FA, ni lazima usajili wachezaji wenye uwezo wa kupambana ili kupata matokeo chanya yatakayosaidia kuwafikisha kwenye mipango na mikakati yao.

Na kama timu yako inahitaji kufika hatua ya nusu fainali, fainali au kutwaa ubingwa wa Afrika, hakuna budi viongozi wa klabu husika kuwekeza katika viwango vinavyofanana na ushindani wa wapinzani ambao wanakutana nao kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Simba, Yanga na timu nyingine za Tanzania ambazo ziko katika vita ya kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa zinatakiwa kusajili wachezaji ambao wana uwezo na uzoefu wa kupambana kwenye michuani hiyo ya CAF na si kuchanganya 'siasa' na uhalisia wa ushindani uliopo katika kufikia malengo.

Naamini zile kanuni zilizowekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuzitaka klabu kusajili wachezaji wa kigeni ambao pia wanacheza katika timu za mataifa wanayotoka, hii itasaidia kuzifanya klabu zetu kuwa imara na zinazocheza soka la ushindani.

Usajili imara ndio njia pekee ya wawakilishi wa Tanzania wanaotaka kutimiza ndoto za kutwaa ubingwa wa Afrika zitatimia na kuwapa furaha mashabiki wa soka wa nchini ambao wanalisubiri taji hilo kwa hamu.

Mbali na kufanya usajili bora, klabu zinatakiwa kuajiri makocha wenye uwezo mkubwa wa kuwavusha na kuwapeleka kule wanapohitaji kufika, kuendelea kusajili wachezaji wa bei rahisi au wa madaraja ya pili, haitakuwa suluhisho la kufikia malengo ya kubeba ubingwa wa Afrika.

Katika kuhakikisha juhudi za kuwekeza kwenye michezo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, huu ni wakati wa viongozi wa klabu kusajili nyota wenye uwezo na kumaliza 'tetesi' zilizopo za 'upigaji' wa fedha kwenye mchakato huo muhimu kwa maslahi ya maendeleo ya soka Tanzania.