Vyoo vya shule kujaa ni hatari kwa wanafunzi

Nipashe
Published at 11:03 AM Apr 09 2024
Vyoo vya shule.
PICHA: MAKTABA
Vyoo vya shule.

KATIKA toleo letu la jana tuliripoti taarifa kuhusu wazazi wa Shule ya Msingi Tembo mjini Songea kutishia kutorudisha wanafunzi shuleni kutokana na vyoo kujaa.

Shule hiyo yenye matundu 10 ya choo, inaelezwa kujaa na kwamba wanafunzi wanalazimika kwenda kujisaidia vichakani.

Walimu pia ambao wanategemea choo hicho nao wanalazimika kwenda vichakani kwenda kujihifadhi.

Kitendo cha kwenda kujisaidia vichakani ni hatari kwa wanafunzi hao kwa sababu wanaweza kukutana na wadudu wabaya na kuwadhuru.

Vile vile, ni hatari kwa afya kwa sababu wanaweza kuambukizana magonjwa ya mlipuko ukiwamo wa kipindupindu au ugonjwa wa matumbo.

Vyoo vya shule kujaa bila hatua kuchukuliwa kwa kuvinyonya ni uzembe ambao hauwezi kuachwa uendelee.

Wanafunzi pamoja na walimu wao wanatakiwa kuwa katika mazingira mazuri ya kusomea na kufundishia.

Mwanafunzi hawezi kuwa makini katika masomo kama atakuwa anataka kwenda kujisaidia halafu anakosa sehemu salama ya kwenda kujisitiri.

 Kwa wanafunzi wa kike ni hatari zaidi kwa kuwa wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi wanahitaji sehemu safi na salama ya kujihifadhi.

Mahudhurio ya wanafunzi shuleni yanaweza kuwa mabaya na kusababisha matokea ya mitihani kutokuwa mazuri kutokana na kushindwa kukosa baadhi ya masomo wanapokuwa kwenye hali ya kujitaji sehemu salama ya kujihifadhi.

Imeelezwa kuwa tangu choo cha shule hiyo kijae ni muda mrefu na viongozi karibu wote wa Manispaa ya Songea wana taarifa zake, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo pia anasema mazingira ya choo ni mabaya kwa sababu matundu yote 10 yameziba na kusababisha haja kubwa kusambaa.

Hii inahatarisha afya za wanafunzi kupata magonjwa ya mlipuko na kama hatua za haraka hazitachukuliwa italeta majangwa makubwa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo amezungumzia licha ya jitihada kuendelea kufanyika baina ya wazazi, uongozi wa shule na serikali kulimaliza tatizo hilo, utatuzi wake una suasua.

Walimu 17 wanaofundisha shule hiyo nao wanategemea kujisitiri kwenye matundu hayo 10 ya choo yanayotumiwa na wanafunzi wa jinsi zote.

Viongozi wa manispaa hiyo wanakiri kuwa hali ni mbaya katika shule hiyo huku wakisisitiza hatua zinachukuliwa.

Moja ya hatua hiyo ni halmashauri kutenga Shilingi milioni tano kwa ajili ya unenzi wa choo na vile vile kuhimiza wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule hiyo kuona umuhimu wa kuchangia ujenzi huo.

Wazazi kwa upande wao toka mwanzo wameonyesha jitihada za kuhamasishana kuchangia ujenzi huo kwa sababu wanaoathirika ni watoto wao na wakipata madhara, gharama za kuwatibu zitakuwa kubwa.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi hao wamedai kuwa pamoja na kufanikisha uchangiaji huo, fedha kidogo iliyopatikana ilielekezwa kwenye chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Fedha kuelekezwa kwenye chakula ni jambo zuri, lakini wanafunzi wakishakula watahitaji kwenda kujisaidia, je wataendelea kwenda vichakani?

Ni vyema zikachukuliwa hatua za haraka wakati ujenzi wa vyoo vingine ukisubiriwa, kujenga vyoo vya muda ili wanafunzi na walimu wao wapate kusitirika na kuepukana na majanga ya kwenda kujisaidia vichakani.