Wanaokwepa kodi katu wasionewe huruma, wanakwamisha maendeleo

Nipashe
Published at 04:50 PM Apr 16 2024
Fedha.
PICHA: MAKTABA
Fedha.

RAIS wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema suala la kulipa kodi ni la msingi kwa taifa lolote na kama jambo hilo halifanyiki, maendeleo yatakuwa ndoto kupatikana. Pia alisema taifa lolote ambalo wananchi wake hawalipi kodi, rushwa huchukua nafasi yake.

Msemo huo wa Nyerere licha ya kwamba miaka mingi imepita, bado una mashiko ndiyo maana mataifa yote duniani, Tanzania ikiwamo, yanahimiza suala ulipaji wa kodi na ndicho chanzo kikuu cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mantiki hiyo, taifa linapokusanya kodi kwa wingi ndivyo kasi ya maendeleo inavyokuwapo. 

Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Tanzania na ile ya Mapunduzi Zanzibar (SMZ) zilianzisha taasisi kwa ajili ya usimamizi wa ukusanyaji kodi na mapato yatokanayo na kodi kama vile za ushuru wa forodha, mafunzo ya ufundi na ongezeko la thamani (VAT) zimekuwa zikitangazwa kuongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa sasa, makusanyo hayo yamepanda kutoka Sh. trilioni 18 mwaka 2021/22 hadi Sh. trilioni 24 mwaka 2022/23.

Makusanyo ya mapato hayo pamoja na yale yasiyo ya kodi, yanayokusanywa katika mamlaka za serikali za mitaa, yamesaidia kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya serikali kama vile barabara, maji, umeme vijijini, elimu na afya. Kadri makusanyo yanavyoongezeka ndivyo kasi ya miradi ya maendeleo pia inavyokuwa. Aidha, bila kodi hakuna maendeleo endelevu. 

Pamoja na jitihada hizo za serikali kusisitiza umuhimu wa kulipa kodi ili kuleta maendeleo endelevu kwa nchi, bado kuna ukwepaji unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na maofisa wa serikali wakiwamo wale waliopewa jukumu la kutekeleza wajibu huo. 

Akizungumza juzi wakati wa Baraza la Eid el Fitr jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuna mtandao wa wafanyabiashara, viongozi wa siasa na maofisa wa serikali wa ukwepaji wa kodi ambao unakwamisha juhudi za serikali katika kufikia malengo ya makusanyo ya mapato na hatimaye kukwamisha shughuli za maendeleo. 

 Rais alisema licha ya ukwepaji kodi kuna wafanyabiashara, watumishi wa serikali wakiwamo waumini wa dini ambao wanachezea mifumo ya kodi kwa lengo la kujinufaisha, hivyo kuwasihi viongozi wa dini kusaidia katika udhibiti wa tatizo hilo. Sambamba na hilo Rais alisisitiza kuwa hata alipomwapisha Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alimsisitiza akusanye kodi na zile za dhuluma aache bali atende haki anapotekeleza wajibu huo. 

Ni dhahiri kwamba kodi ni msingi mkuu kwa maendeleo ya taifa lolote na kama suala hilo halitasimamiwa ipasavyo, kuna hatari ya kuporomoka kwa uchumi kunakoendana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa. Ukwepaji kodi una madhara makubwa lakini pia matumizi ya nguvu katika ukusanyaji wa mapato hayo ya serikali ni chanzo cha kuwapo kwa tatizo hilo. 

Ukwepaji kodi au kuchezea mifumo ya kodi ni moja ya vitendo vinavyohesabika kuwa ni uhujumu uchumi kwa sababu mtu anapofanya hivyo, ama kuingiza bidhaa kwa njia ya magendo au kushirikiana na maofisa wa serikali kufanya udanganyifu wa aina yoyote, haikubaliki hata kidogo. 

Kama alivyoagiza Rais Samia, ni vyema viongozi wa dini wakalisisitiza jambo hilo kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa taifa. Viongozi wa dini wanapaswa kukemea vitendo hivyo kama wanavyofanya katika masuala ya ufisadi, rushwa, katiba mpya,  ukatili na ndoa za jinsia moja.

Kutokana na umuhimu wa kodi kwa maendeleo, wale wote wanaobainika kukwepa kodi wachukuliwe hatua kali za kisheria na ikiwezekama sheria zibadilishwe ili kuwabana zaidi na kuwaadhibu watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.