Fahamu jinsi nyangumi wanavyozungumza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:17 AM Apr 16 2024
Nyangumi akiwa na mtoto wake.
PICHA: MAKTABA
Nyangumi akiwa na mtoto wake.

ILIKUWA mwaka 2021, nje ya pwani ya Kusini-Mashariki mwa Alaska, timu ya wanasayansi sita ilicheza rekodi ya sauti ya salamu kupitia spika iliyo chini ya maji.

Walipigwa na butwaa walipogundua nyangumi mmoja waliyemwita Twain, alipojibu sauti hiyo. "Ni ajabu," anasema Josie Hubbard, mtaalamu wa tabia za wanyama katika Chuo Kikuu cha California, Davis ambaye nae alikuwa kwenye chombo hicho.

“Lazima uzime chombo umbali wa mita kadhaa walipo nyangumi. Katika tukio hili, Twain mwenye umri wa miaka 38 alikwenda kwenye chombo, na kukizunguka kwa dakika 20,” anasema Hubbard.

Twain alipoondoka, Hubbard akaenda chini ya chombo na ndipo wakagundua nyangumi huyo alikuwa akijibu sauti ya spika kwa dakika zote 20. Sauti ndefu inayokuja na kupotea, ikiwa na mapigo na milunzi.

Wanasayansi waliweka vifaa vya kurikodi baharini ili kukusanya sauti za nyangumi, ambaye akaonyesha orodha ndefu ya tabia zinazofanana na za wanadamu. 

Wanashirikiana wenyewe na viumbe wengine, huku wakifundishana stadi za maisha, kama kutunza watoto na kucheza.

Tofauti na wanadamu, inaelezwa wanatumia zaidi sauti kuliko macho kwenye mambo yao mengi. Sauti zao zinaweza kusafiri mbali na kwa kasi ndani ya maji kuliko inavyosafiri hewani.

Nyagumi aina ya Cetaceans kwa mfano, wanaelezwa hutegemea kelele kuwasiliana wenyewe, kusafiri, kutafuta wenza na chakula, kulinda maeneo na rasilimali zao na kuepuka wanyama wanaokula wenzao.

Watoto wao wanatajwa nao hulia kama watoto wachanga wa binaadamu, wengine wanaaminika kuwa na majina na makundi yao kutoka sehemu tofauti za bahari huwasiliana lugha za eneo.

Nyangumi husikika wakiiga lahaja za vikundi vya kigeni- na wengine wanadhaniwa kuiga hata sauti ya kibinadamu.

REKODI ZAO

Rekodi ya kwanza ya nyimbo za nyangumi ilipatoka anarekodiwa mwaka 1952 na Mhandisi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Frank Watlington.

Takriban miaka 20 baadaye, mwanabaiolojia wa baharini Roger Payne akagundua sauti hizo zilipangwa kwa kujirudiarudia. 

Hilo hubadilisha uelewa wa sauti za nyangumi na kuzua shauku iliyowapeleka miongo kadhaa ya utafiti.

KINACHOFUATA

Watafiti wanatumai kuchambua sauti za nyangumi kunaweza kusaidia kuelewa sauti zao. Watafiti wanadhani kuwa sauti za nyangumi zina ujumbe wenye maana.

Hata hivyo, wanasema uelewa wetu wa mawasiliano ya nyangumi bado uko katika hatua ya awali sana.

Ni katika kipindi chote cha kubadilishana sauti, Twain kila mara akaitoa sauti kama iliyotoma katika spika na kila baada ya sekunde 10, naye akatoa sauti hiyo. Hiyo ilifanywa mara 36 kwa dakika 20.

"Changamoto kubwa kwetu ni kuelewa sauti hizo na kuamua maana yao, ili tuweze kujua maana. Nadhani AI itatusaidia kufanya hivyo," anassema Brenda McCowan, Mtafiti katika timu hiyo.

Umbali wa zaidi ya kilomita 8,000, kundi la wataalamu wa akili bandia, lugha asilia, waandishi, wataalamu wa lugha, wanabiolojia wa baharini, wataalamu wa roboti - wanatarajia kutumia AI - kufafanua sauti za nyangumi.

Timu hii nyingine ilizinduliwa mwaka 2020, Ceti (Cetacean Translation Initiative), ikiongozwa na mwanabiolojia wa baharini David Gruber, imekuwa ikirekodi kundi la nyangumi katika pwani ya Dominica, kisiwa cha Karibea, kwa kutumia maikrofoni kwenye maboya, samaki wa roboti na vifaa vilivyowekwa kwenye migongo ya nyangumi.

"Ni vigumu kwetu kuelewa ulimwengu wao, zaidi ya maingiliano haya mafupi sana ya sauti. Huyu ni kiumbe wa kipekee, mpole, na kuna mengi tu yanayoendelea katika maisha yake," anasema Gruber.

"Kila wakati tunapotafiti, tunapata utata na namna mpya zaidi katika mawasiliano yao."

Anaamini baadaye kutafikiwa hatua ya maendeleo ya kiteknolojia, kuwezesha mawasiliano na nyangumi.

Hadi sasa, taarifa zilizokusanywa zinafanyiwa uchambuzi kwa kutumia mashine, kugundua maana ya sauti hizo, na matokeo yanatarajiwa kutolewa mwaka 2024.

Samantha Blakeman, Meneja wa Data za Baharini wa Kituo cha Kitaifa cha Oceanography, ana ufafanuzi: "AI inaweza kuturuhusu kuelewa mifumo ya mawasiliano ya viumbe vingine vingi.

“Nadhani litakuwa jambo zuri kwa ulimwengu - ikiwa tunajali kuhusu kile ambacho nyangumi wanasema."