Ilivyo DRC yenye maafa, wakimbizi, shule na jimboni Kivu zimefungwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:54 AM Apr 17 2024
Ndivyo yalivyo madhila wanayopata wakimbizi wa vita, huko Goma, DRC.
Picha: Maktaba
Ndivyo yalivyo madhila wanayopata wakimbizi wa vita, huko Goma, DRC.

SIMULIZI si nzuri maana ilikofika, askari wa Kitanzania watatu waliokuwa sehemu ya vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), pia mwenzao mmoja wa Afrika Kusini wameuawa.

Leo hilo lina wiki moja, ikiakisi uhalisia wa hali mbaya iliyoko DRC, hata katika jimbo la Kivu penye mapigano kati ya vikosi serikali na waasi nchini humo. Mapigano yasiyoisha miongo kadhaa, mashambulizi hasa kutoka waasi wa M23. 

Tangu mwezi Desemba mwaka jana, SADC imepeleka kikosi mkoani Kivu Kaskazini, kinachoundwa na wanajeshi kutoka; Afrika Kusini, Tanzania na Malawi kusaidia vikosi vya serikali ya DRC kupambana na waasi hao wa M23, inayodaiwa kusaidiwa na Rwanda, huku yenyewe ikikanusha vikali. 

Ni suala tata kwani kabla ya vikosi hivyo vya SADC, pia wakawapo wenzao waliofika kwa madhumuni hayo, kisha wakaondoka kutokana na madai ya kiwango cha uwajibikaji wao.

Mwanzo, SADC ikatangaza kuuawa askari wake, mnamo Februari 15 wakati wanajeshi wawili wa Afrika Kusini walipouawa kwa bomu karibu na Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hayo yanaendelea, huku kwa wenyeji hali ni mbaya, kundi kubwa la wakimbizi na matokeo ya vifo, hata sikukuu za Pasaka na Iddi Elfitri zilizopita hivi karibuni, wenyeji walinukuliwa kuona kama haiwahusu, wako katika shida.

SHULE ‘ZABUMA’

Kuna vilio tangu mwezi uliopita, kwamba hali ya wakimbizi wa vita vya M23, wanaokwepa hali mbaya. Sasa imeathiri mno ustawi wa elimu katika mji wa Goma, baadhi ya shule zinashindwa kuendesha masomo kwa sababu ya ugeni wa wakimbizi katika majengo yao. 

Wanafunzi wanaomimika Goma, wanakimbia mashambulizi ya vikosi vya DRC na waasi wa M23, wakizuia masomo kuendelea.

Wakimbizi hao walioingia katika mji wa Goma, wengi sasa wamejazana kwenye madarasa ya shule, hali iliyotajwa mwezi uliopita kuzuia kalenda za masomo. 

Mmiliki wa Shule ya Msingi Lac Vert, Hangi Bahati, akabainisha kuwa tangu wakati huo, watoto wamekuwa mitaani, akiwa na ufafanuzi:  

"Kupitia vita watoto kwa leo hawako tena ndani ya masomo. Masomo (shule) imebaki ni ‘ma- camps’ (kambi) ya majeshi na watoto leo wanazunguka mitaani, sababu ya vita hawana walimu!..."

Mamlaka ya elimu ya msingi mkoa wa Kivu Kaskazini, inasema elimu imeathirika kitaifa, Ofisa Mkuu wa Elimu Kaskazini mwa Kivu, Luc Baweza Kabango, naye anaelezea: 

"Tangu vita vilipoanza zaidi ya miaka miwili iliyopita, utaona kwamba mambo yanabadiliki, yaani shule nyingi zimefungwa na kuna watoto ambao hawasomi. 

“Itabidi tufanye kazi kubwa kwa sababu akili za watoto zinaathiriwa na migogoro ya silaha, kuna watoto wengine ambao pia watakuwa kama wanyama au waasi. Hii inaharibu vipengele vyote vya elimu,” analalamika.

Mjini Goma, wapiganaji wa M23 wanaendeleza mashambulizi kwenye maeneo ya; vijiji vya Katanda na Mayi ya Moto, vilivyoko kilomita chache kutoka Vitshumbi sasa wanapadhibiti.

Wiki tatu ziliyopita, serikali imewataka wakimbizi waliokimbilia kujisitri shuleni waondoke, kuruhusu watoto kurejea shuleni masomo yaendelee.

Hata hivyo, wazazi wa wazazi wa watoto bado wanakabaki na wasiwasi ya hali hiyo, hata kuwazuia watoto kubaki nyumbani wasiende shule, hadi watakapohalikisha mustakabali mzuri wa kiusalama.

Bora Batende, ni mzazi wa mwanafunzi mmoja na ambae anayesema kabla ya vita, wanawe ilikuwa wanasoma na kutokana na hali hiyo amewazuia.

Watu waliokimbia vita, pia nao wanaishi shuleni kwenye madarasa wakisema wanapenda kuondoka katika makazi hayo shuleni, ila hawana mbadala pa kwenda, pia hata hawana vifaa vya kujenga mahema ya muda katika kambi walizoelekezwa. 

Mkimbizi Bibiche Ndoole, ana maelezo yake kwamba:"Tulikimbia vita vya M23, tuliona mashambulizi yanakuwa mengi, ndugu zetu wengi wameuawa, ndio sababu tukakimbia na kuja kujihifadhi hapa shuleni. 

“Kwa sasa tunashindwa kujua mahala pa kwenda, tunafahamu wanafunzi wa hapa Mugunga hawawezi kusoma kwa sababu yetu."

MACHUNGU HALISI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), tayari mwezi uliopita likataja watu milioni 5.7 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani Mashariki mwa DRC.

Aidha, kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo, Mathew Saltmarsh jijini Geneva Uswisi, ni kwamba imeshatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kutokana na ongezeko la hatari kwa watu waliokimbia makazi yao Mashariki mwa DRC, 

Hiyo inapokewa na kauli ya baba wa watoto sita, anayetafuta usalama kwa familia yake katika eneo la makazi ya muda karibu na Goma, baada ya mkewe kuuawa na bomu huko Sake, jimbo la Kivu Kaskazini.

“Miaka miwili ya mizozo katika maeneo ya Kivu Kaskazini huko Rutshuru na Masisi, imewalazimu zaidi ya watu milioni 1.3 kukimbia makazi yao ndani ya DRCna kusababisha jumla ya watu milioni 5.7 kuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri,” inaeleza UNHCR.

Msemaji huyo anaongeza kuwa, tangu mapigano makali yashike kasi katika mji wa Sake, tarehe 7 Februari, karibu watu 300,000 wamewasili katika jiji la Goma, ambako hali ilikuwa mbaya. 

Watu zaidi ya 85,000 walikuwa wamekimbia ghasia hizo hizo na kutafuta makazi katika eneo la Minova la Kivu Kusini, ambalo tayari lilikuwa limepokea watu 156,000 waliokimbia makazi yao tangu Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa UNHCR, kuna shambulio la makombora katika kituo cha biashara lililofanyika Machi 20, hata likamuua mwanamke mkimbizi wa ndani na kuwajeruhi wengine watatu, wakiwaemo watoto wawili.

Ripoti za milipuko ya mabomu ya kiholela huko Sake na Goma katika wiki za hivi karibuni, imeshaua zaidi ya watu 30 na kujeruhi takriban 80, hadi wiki tatu zilizopota.

Mwaka jana kuna shule 25 zilichukuliwa na vikundi vyenye silaha visivyo vya serikali katika maeneo ya Masisi na Rutshuru pekee, na zingine 17 zilishambuliwa. Mwaka huu, pia shule saba zimeharibiwa na milipuko ya mabomu.

Pia mwaka jana katika eneo la Kivu Kaskazini pekee, UNHCR inaripoti mikasa 50,159 zilizoripotiwa za unyanyasaji kijinsia, zaidi ya nusu ya nusu ni ubakaji, ndai yake asilimia 90 ya waathirika walikuwa wanawake na wasichana, wakati asilimia 37 ni watoto.

Hilo linaifanya UNHCR kukemea kukomeshwa moja kwa ghasia hizo, ikizitaka pande zote katika mzozo kuheshimu na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, kwa kuwalinda raia.

Pia, inataja hifadhi ya kibinadamu ziliongezeka katika majimbo ya Mashariki, ikitolewa takwimu kati ya Juni na Desemba mwaka jana, msaada wa kuokoa maisha ulifikia zaidi ya watu milioni 3.1.

UNHCR imetoa hifadhi ya dharura kwa zaidi ya watu 40,000 walio katika mazingira magumu  waliofika Goma.

ILIKOTOKA DRC

Kijiografia, ina mji mkuu Kinshasa. Ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika na 11 duniani, wakazi wake wanakadiriwa milioni 12, umaarufu wao duniani, magwiji wa muziki wa dansi.

 Hata hivyo, tangu kupata uhuru mwaka 1960, hawajawahi kufadi utulivu na amani ya kudumu. Majirani wao ni mataifa; Jamhuri ya Afrika ya Kati, Zambia, Rwanda, Burundi, Angola na Tanzania kupitia Ziwa Tanganyika.

Wakati inapata uhuru iliitwa taifa la Congo, ikiongozwa na Waziri Mkuu, Patrice Lumumba. Hakudumu, aliuawa katika mapinduzi, nafasi yake ikachukuliwa na Mobutu Sese Seko Wazabanga Kuku, mwaka 1965. 

Mwaka 1971, Rais Mobutu akabadili jina la nchi kuwa Zaire, akiendelea na utawala uliotajwa wa kidikteta hadi mwaka 1997, alipong’olewa na wana -mapinduzi waliojipanga nje ya mipaka, wakampa urais, mpambanaji mwenzao na mkazi wa Dar es Salaam, Laurent Desire Kabila.

Hapo naye akabadili jina la nchi kuwa DRC, akidumu madarakani hadi mwaka 2001 alipouawa na mmoja wa walinzi wake.

Ni hali iliyochangia machafuko mengi ndani ya nchi, kukiwapo makadirio kati ya mwaka 1998 na 2003 kumesababisha vifo vya watu milioni 5.4.

Ni wakati ulioshuhudiwa vikundi vingi vya waasi, vikileta machafuko makubwa ya kisiasa, badhi ya waliomuunga mkono Marehemu Mzee Kabila, Profesa Wamba Dia -Wamba, ambaye akamuasi na kujiunga na kikundi cha uasi Rally for The Congolese Democracy (RCD), ambacho kikapatwa na msuguano wa ndani kuzaa, RCD - Goma na RCD -Kisangani, iliyoongozwa na Wamba.

Pia, kukawapo kikundi kingine kilichosumbua DRC kupigana nayo chini ya muasi, Dk. Bizimana Karahamuheto au umarufu wake Bizima Karaha, anayedaiwa na unasaba wa uraia jirani, alianza uasi mwaka 1998 dhidi ya Rais Laurernt Kabila, baadaye aliposhindwa akakimbilia nchini Afrika Kusini.

Taifa likiwekwa chini ya mwana wa Laurent Kabila, aitwaye Joseph, mwanafuzi wa Shule ya Sekondari ya jioni Zanaki (iliyokuwapo wakati huo) jijini Dar es Salaam na Sangu ya Mbeya kwa kidato cha tano na sita, akaongoza nchi kuanzia mwaka 2001 hadi 2019.

Ni zama zinazotajwa, akafanikishaa kutimiza hali ya hewa ya vita na hata akaondoka madarakani, kwa kuwezesha kuwapo uchaguzi wa amani wa kwanza DRC, mwaka 2018 tangu uhuru wake akimuachia madaraka.

Hata hivyo, ukanda wa Mashariki ya Congo, ambako kunazugumzwa Kiswahili, kumebaki na historia ya chokochoko ikishuhudiwa zaidi tena kuanzia mwaka 2015, hali inayoendelea hadi sasa.

Vita hivyo, vyanzo vya vita visivyoisha vitanja kuzaliwa na mambo mawili: Moja, ni lile o Rais Tshishekedi, aliye madarakani kwa awamu ya pili, baada ya kushinda uchaguzi karibuni, anaishutmu majirani – Rwanda.

Liingine  ambalo ndilo kuu, unatajwa utajiri wa madini na hasa shaba, mataifa ya kigeni na matajiri  yakielezwa wana mkono kama ngazi ya kufikia rasilimali hiyo.

Ni utajiri unaopatikana katika majiji yake makubwa kama Kinshasa, unaoufutiwa na Lumubashi,wa tatu, Mbuji Mayi.

Raia wake wamekuwa wakitapatapa, huku Umoja wa Mataifa katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu, inaitaja DRC kushika nafasi ya 179 kati ya 191 kimaendeleo. Kuna raia 600,000 wanaotajwa kuishi nchi jirani na watu milioni 4.5 wamehama makazi yao.