Siasa za Samia zinavyovuka na mitaji ya historia awamu tano zilizotangulia

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 06:46 AM Apr 17 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Picha: Maktaba
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

MARA alipoingia madarakani, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan miaka mitatu na miezi kadhaa sasa akaja na kaulimbiu ‘Kazi Iendelee. ’Awali akiwa mkuu wa pili wa nchi, alikuwa sehemu ya kaulimbiu ‘hapa kazi tu.’

Je linapokuja swali la kumtafsiri kisiasa, Rais Dk. Samia, anayetumikia awamu ya sita sasa, anasimama wapi, jibu linaangukia tafsiri mtambuka.

Mosi, ni mtaalamu wa Utawala, pia Uchumi wa Maendeleo. Daima, safari yake yote, hajawahi kuwa nje ya maeneo hayo, ingawa ninamuongezea taaluma ya matendo na falsafa zake tatu.

Mara zote yu muumini wa fani Mazingira, eneo alilodumu nalo sana katika utedaji serikalini, vilevile akibaki kuwa Mama wa kwanza kushika usukani wa kuongoza nchi, daima hajakaa mbali, anadumu kwa matendo katika haki za kijinsia na vijana.

Kimsingi, Dk. Samia anatumikia Awamu ya Sita sasa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoendelea kushika nafasi, hivyo itikadi, sera na ilani zake zina mfumo wa kudumisha ya CCM.

Je kisiasa yu wa namna gani? Dk. Samia ni muumini wa kuendeleza ya chama chake – CCM, hali kadhalika ‘kazi inaendelea’. Hapo katika Awamu ya Tano alikuwa sehemu ya kubuni na kuyasimamia.

Mbali na mradi mkubwa, reli ya SGR na Bwawa la Umeme Mwalimu Nyerere, ilianza kutekelezwa katika Awamu ya Tano, safari zake ni za mbali.

Bwawa la Mwalimu Nyerere likiwa na chimbuko la Awamu ya Kwanza, huku SGR dodoso zake zikaanza katika Awamu ya Pili, kwa Rais Jakaya Kikwete zote sasa ni ‘bidhaa’ za Awamu ya Sita.

Ni katika eneo hilo, Rais Dk. Samia, anaonekana kuwa na chembe za Rais Mzee Ali Hassan Mwinyi, pia za Rais Kikwete.

Staili yake ya uongozi kisiasa amekuwa akitumia zaidi mfumo wa maridhiano na kuelewana kisiasa, na hiyo ikaonekana mapema tu baada ya kuingia madarakani Januari mwaka 2021, akatamka kuja na falsafa hiyo ya maridhiano. 

Hizo akazitaja kwa Kiingereza; ‘reconciliation, resilience, reforms na rebuilding’, akimaanisha ‘upatanishi, ustahimilivu, mabadiliko na ujenzi upya’.

Hayo muda mfupi baadaye akaonekana kuanza kuzitelekeza katika matukio mbalimbali kama vile kufungulia mjumuiko wa kisiasa uliokuwa umezuiwa na kuachiwa washitakiwa wa kisiasa.

Vilevile, kuna mjumuiko katika ulingo wa siasa kwa vyama hasimu, kama vile kuwa anapokuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CHADEMA.

Hadi sasa Rais, Dk Samia, pia ni Mwenyekiti wa CCM, amekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono vyama vya upinzani katika kulisukuma dai lao kuu la kuandikwa Katiba Mpya.

Ni mtazamo ukaonyeshwa kwa kiasi kikubwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM, aliyeukaribisha mfumo huria kiuchumi mwaka 1985 na mwaka 1992, akawezesha mabadiliko kisiasa.

Kisheria, nchi ikaingia katika siasa ya vyama vingi; ikibeba sura kuu ya maridhiano ya utashi tofauti wa kisiasa nchini na hata kukashuhudiwa uchaguzi wake mwaka 1995 tangu ifungwe kisheria mwaka 1964.

Tena, Dk. Samia anashabihiana katika dhana maridhiano na Rais Kikwete, akifungua mlango wa mjadala wa Katiba Mpya, hata akaliundia bunge maalum, ingawaje halikufika mbali. 

Samia ndiye aliongoza Bunge la Katiba, kikao kilichompa sifa na heshima anayodumu nayo hadi sasa, kutokana na umahiri na busara zake kazini, akiwa mezani pale kikaoni Dodoma.

Sambamba na hayo, kama inavyojulikana uongozi wa siasa unavyohitaji ustahimilivu, mifano ya yaliyofanywa na Mzee Mwinyi na kijana wake Kikwete, unasaba wake uko wazi sasa katika nyendo zake Rais Dk. Samia.

NGOME YA MAENDELEO

Katika safari ya maendeleo, anaonekana kubebwa kwa ‘kazi iendelee’, yake mambo yaliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere katika Mpango wa Maendeleo ya Nchi ya Kwanza wa mwaka 1964 hadi 1969.

Hizo ni kuwatosheleza Watazania hasa katika mahitaji ya Elimu, Kilimo na Afya na marais wa awamu zote zilizomtangulia, hawajawahi kuziacha.

Mathalan, mikakati ya kilimo nchini ambayo Rais Nyerere, pia elimu ya msingi, Rais Mkapa akaelekeza nguvu katika kuboresha na kutanua wigo, Rais Samia sasa amezama katika kuongeza mtaji wa kibajeti na kilimo cha kisasa. 

Ndio picha inayofanya kilimo cha Kitanzania kikiwekezwa bajeti maradufu kutanua umwagiliaji, soko la mazao kama ya ufuta, miradi maalum ya kuingiza vijana katika ajira ya kilimo cha kisasa, huku mbolea ikikuzwa maradufu kwa viwanda nchini ikiwa na wakala mpya.

Rais Dk. Samia mwenyewe amekuwa akinadi kilimo nchini nje ya mipaka kuanzia soko, hadi ukaribishaji mitaji, ili kuleta mapinduzi kilimo alichotetea Mwalimu Nyerere kwa dhana “kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa.’

Hiyo ndiyo inayoangaliwa katika maboresho ya Sekta ya Elimu, kuanzia mfano Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na kama huo wa sekondari uitwao MMES, katika Awamu ya Tatu, Rais Kikwete akabuni Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), vyote sasa Rais Samia anaviendeleza, kama miradi mikubwa kitaifa.

Ushahidi wake uko katika idadi zaidi ya zahanati na vituo vya afya 300 kuona zinafikisha huduma katika kata, vilevile sera hiyo katika shule, MMEM na MMES ikiboreshwa, sasa shule maalum za wasichana na utatuzi wa kero na mahitaji shuleni zikibeba ajenda kubwa.

Kiuchumi, wakati Mzee Mwinyi akaonyesha wazi kuwa muumini mkubwa wa ushirikishaji sekta binafsi, mrithi wake Rais Mkapa, akaunda Tume ya Rais ya Kubinafsisha Mashirika ya Umma (PSRC). Kinachofanyuwa sasa katika Awamu ya Sita, ni kuzipa nafasi sekta binafsi, inayoakisi matendo hayo ya wakuu wa Awamu ya Pili na Tatu.

Hiyo inamfanya Rais Dk Samia, kuwa madarakani leo ana sura zote zilizotangulia na falsafa ya kubeba chama chake, ikithibitisha kaulimbiu ‘kazi iendelee’ na ndio maana miradi mikubwa kitaifa imo Bwawa la Mwalimu Nyerere na SGR, ya Awamu ya Tano.

Pia, inaungana na ‘Elimu Bure’ ambayo imeboreshwa maradufu katika awamu yake, kuwezesha Watoto wa Kitanzania kunufaika na elimu yao, kuanzia ngazi ya shule hadi vyuo, mtaji wao sasa ni juhudi zao  kuelekea kufaulu masomo.