Ubadilishaji uzio, samani, matundu vyoo inavyobadilisha elimu Ubungo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:12 AM Apr 16 2024
Mbunge Kitila Mkumbo akizungumza na wanafunzi.
PICHA: MAKTABA
Mbunge Kitila Mkumbo akizungumza na wanafunzi.

KATIKA kipindi cha miaka mitatu Jimbo la Ubungo limepokea jumla ya Sh. milioni 236.9, kwa mujibu wa Mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ikimletea mabadiliko makubwa katika mfumo wake wa elimu

Mbunge Kitila, mzizi wa taaluma yake amesomea ualimu na talauma yake ikadumu darasani, kabla kubadili mwelekeo wa ajira alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Baadaye akajiunga na siasa, tayari akiwa wa wasifu wa profesa, anayewasuka walimu watarajiwa, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Sifa ya matokeo yake sasa, imekomboa shule ambazo zilikuwa hazina uzio na geti na kuchangia kuwapo kwa mwingiliano wa watu, pindi watoto wakiwa darasani.

Fedha nyingine zinatajwa kutawanywa katika miradi mbalimbali iliyoko katika kila kata jimboni humo katika sekta ya uchumi, miundombinu na masuala ya kijamii.

Pia, inatajwa fedha kutumika kukamilisha ujenzi na ukarabati wa baadhi ya vituo vya polisi. Kielimu, fedha za Mfuko wa Jimbo zimetumika kujenga uzio katika baadhi ya shule za msingi jimboni humo zikiwamo Makuburi, Kilimani, Uzuri, Mpakani, Mabibo na Mugabe, huku Shule ya Amani ikikarabatiwa na Kawawa kujengewa matundu ya vyoo.

SAUTI YA SHULENI

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makuburi Hussein Dadi, anabainisha kuwa, uzio pamoja na geti lililowekwa limewasaidia kuondokana na mwingiliano baina ya wanajamii na shule.

“Wakati kukiwa hakuna uzio watu walikuwa wakikatiza maeneo ya shuleni muda ambao watoto wanaendelea na masomo, hivyo kuchangia kutokuwapo kwa wanafunzi.

“Kuna wananchi walikuwa wanapita muda wote. Mafundi magari walikuwa wanaleta magari mpaka kwenye eneo la shule na kusababisha kelele na kuondoa utulivu kwa wanafunzi na wakati mwingine usalama wa watoto ulikuwa mdogo,” anasema Mwalimu Dadi.

Wanafunzi shuleni hapo, Anna Lutamboka na Hassan Juma, wanasema changamoto ya mwingiliano wa watu shuleni hapo ulikuwa ukiwaathiri katika masomo yao.

Katika ufafanuzi wao wanatamka, kuwapo kwa uzio na geti, kumechangia pia kupunguza utoro wa wanafunzi wakati wa masomo kwa kuwa kwa sasa ili watoke ni lazima wapiti getini.

Ni kauli inayoungwa mkono na naungwa mkono, pia wanafunzi wa Shule ya Msingi Mugabe iliyopo jimboni humo, wanafunzi Amini Jackson, Anita Richard na Jacklin John, wanaeleza kabla ya ujenzi wa uzio, walikuwa na changamoto kuibwa mabegi yao na watu wa nje, sasa wapo salama.

Mafanikio mengine anayataja katika sekta hiyo jimboni humo, ni pamoja na ununuzi wa samani za walimu zilizohusisha shule za msingi ambazo ni.

Hapo kunatajwa:  Manzese (viti 18), Ukombozi (viti 18), Mianzini (viti 14) na Shule za Sekondari Mburahati (viti 16) na ya Kimara (viti na meza moja).

Shule nyingine za msingi zilizonufaika na samani ni : Golani, Golani B, Kilungule, Kimara Baruti, Millenia ya Tatu na Msewe (viti 26). Huk kuimenunuliwa vifaa; Laptop, zulia ofisi ya mwalimu mkuu, kifa acha cha kuhufadhi nyaraka, kabati na mapazia.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Urafiki, nao wanaatajwa kunufaika kwa kupatiwa madawati 120 yaliyoondoa changamoto yao, huku Shule ya Sekondari Mburahati, ikipatiwa madawati 93 na meza 93 za wanafunzi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mianzini, Elizabeth Kambi, anasema kabla ya kukabidhiwa samani hizo iliwalazimu wanafunzi kuchangia viti, jambo lililowasababishia usumbufu.

“Mwalimu ukiacha kiti unakuta mwanafunzi kakibeba kaenda kukalia. Hii ilikuwa changamoto kubwa ambayo iliondoa umakini katika kazi na kutupunguzia ufanisi. Kwa sasa viti vya walimu haviingiliani na vya wanafunzi,” anaibainisha Mkuu wa Shule Elizabeth.

ANAVYONENA MBUNGE

Mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo ambaye pia, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, anasema aliamua kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuratibu na kusimamia fedha za Mfuko wa Jimbo pamoja na miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za mfuko huo.

Prof. Kitila anasema aliamua kuliacha jukumu la kuratibu fedha za mfuko wa Jimbo kwa kamati maalum ya mfuko wa jimbo ili kuweka usimamizi mzuri na mgawanyo wa fedha hizo katika kutekeleza miradi.

“Nilifanya hivyo kwa maana, kamati hii inahusisha madiwani na wataalamu wa kada mbalimbali kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

“Nilipoingia madarakani niliamua kuunda Kamati ya Mfuko wa Jimbo ili kuwapa majukumu ya usimamizi wa fedha na miradi inayotokana na mfuko huu.

“Fedha za mfuko wa Jimbo zinatolewa kwa ajili ya kuchochea maendeleo pale ambapo wananchi wanakuwa wameanzisha jambo lao tumekuwa tukiwashika mkono kwa kumalizia,” akabainisha Prof. Mkumbo.

Anasema mambo mengine ya kijamii yaliyofanyika kwa lengo la kugusa maisha ya wananchi aliyataja ni pamoja na ujenzi wa vizimba vya mama lishe katika Soko la Mawasiliano, kuchochea shughuli za kiuchumi kwa vijana wa Kata ya Makuburi na shughuli za kiuchumi kwa wanawake wa Makurumla.

Jimbo la Ubungo ni miongoni mwa majimbo 10 yaliyoko mkoani Dar es Salaam likiwa katika wilaya ya Ubungo yenye majimbo mawili ya Ubungo na Kibamba. 

ULINZI NA USALAMA

Kuna mazao yanayovunwa zaidi ya lengo kuu la kuboresha elimu. Hapo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mavurunza, Taji Kanuti, anasema kuanza kufanya kazi kwa Kituo cha Polisi Mavurunza kumesaidia kuongeza utulivu na ulinzi katika Kata ya Kimara na maeneo jirani kutokana na kituo hicho kuwa kikubwa.

“Kilichukua muda mrefu kujengwa, lakini kwa awamu yake kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo, fedha zake binafsi pamoja na wadau wengine kimekamilika,” anasema Kanuti.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Sophia Fitina, anasema kuwapo wa Kituo cha Polisi Kibo, ni msaada mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo na utasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu kwa kuwa, awali walikuwa wakifuata huduma za polisi katika Kituo cha Polisi Kimara Mwisho, ambako ni mbali na mtaa wao.

Diwani wa Kata ya Kimara, Ismail Mvungi, amepongeza kazi kubwa iliyofanyika na kutaka wananchi kulinda miundombinu iliyotengenezwa kwa kuifanyia ukarabati pale inapoharibika.

“Hii miradi imeshakabidhiwa kwetu hatuna budi kuitunza na kuifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili idumu na kuendelea kutusaidia,” anasema.

Diwani wa Kata ya Makuburi, Olver Shirima, anasema katika eneo lake kumejengwa vivuko viwili cha Mikongeni na Uluguruni ambavyo vimesaidia wananchi kuondokana na adha waliyokuwa wakiipata awali.

Anna Esau, Amina Hamis na Mjuni Mjunwa ni wakazi wa Kata Makuburi ambao wanaeleza kuwa, kivuko cha Mikongeni na kile cha Uluguruni vimeondoa changamoto kwao, kwani wakati wa mvua walishindwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na kutatika kwa mawasiliano.

Diwani wa Kata Sinza, Raphael Awino, anaeleza kuwa Mtaa wa Nungunungu Sinza E, umejengewa mtaro na kivuko cha waenda kwa miguu pamoja na ujenzi wa barabara ya Sinza E na B ukiwa katika hatua za awali.

Sekta nyingine ambazo zimeguswa ni ukarabati zikiwamo Ofisi za Mitaa ya Uzuri na Kilimani Kata ya Manzese, Ofisi ya Mtaa wa Jutegemee, Kata ya Mabibo, Ofisi ya Mtaa wa Kimamba, Kata ya Makurumla na Ofisi ya Mtaa wa Kisiwani, Kata ya Mburahati.

Pia, kumefanyika ujenzi wa vivuko katika maeneo mbalimbali hasa yale ambayo yaliyokuwa na changamoto ya mawasiliano kipindi cha mvua.