Ufunguo anaotumia Rais Samia kusuka elimu kwa mahitaji ya leo

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 09:07 AM Apr 16 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wanafunzi wasichana, alipokuwa ziarani  mkoani Lindi.
PICHA: MAKTABA
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wanafunzi wasichana, alipokuwa ziarani mkoani Lindi.

JUMANNE iliyopita mada gazetini ilijadili nafasi ya mwalimu na mwanafunzi kuwa ndio nguzo ya kwanza katika taaluma wakati wa kufanikisha elimu, mafanikio yake yakiungwa na msamiti ‘ukiona vinaelea vimeundwa.’

Mafanikio ya moja kwa moja upande wa mwalimu darasani, huwa nyuma yake kuna mchango wa serikali ikimtetea. Vivyo hivyo, mwanafunzi akisimamiwa katika maeneo ya kila siku na wazazi au walezi.

 Serikali inapowekeza katika kuelimisha na ajira ya wataalamu wanaoingia darasani kufundisha, ujenzi wa madarasa na mahitaji ya kitaalamu yanajibu kuboreka elimu ya anayefunzwa darasani, pia mfundishaji akitanuka kifikra.

Mwalimu ni mfanyakazi, anapaswa kuthaminiwa kwa mahitaji yote muhimu ya kimaslahi kama mshahara, posho na huduma; makazi na tiba. Anatulia kifikra na tija yake darasani inakuwa juu.

Wazazi na walezi, hao wanaangukia katika wawezeshaji wakuu ‘namba moja’ nje ya darasa. Mahitaji yote ya kisheria, kisera na kimila kwa mwanafunzi kama vile muda wa mwanafunzi kusoma, mahudhurio yake shule, pia kuhudumia mahitaji kama sare na madaftari.

Hiyo huenda mbali katika mahitaji mahsusi na maelekezo ya kishule, kisheria na kiserikali kama vile njia maalum za kumlinda mwanafunzi wa kike, ni jukumu lake mzazi kuanzia nyumbani na anaikabidhi shule, pale mwanafunzi anaingia ndani ya geti lake.

Wakati wote huo, nyuma ya pazia mamlaka ya kiserikali inaangalia kuhakikisha shule na wazazi hawatoki nje ya msimamo.

DARASA LA SAMIA

Hivi karibuni nchini ilifuatiliwa kwa kina, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya uwekezaji mkubwa kiserikali katika elimu nchini na amefanya hilo, kulingana na mahitaji ya sasa kielimu, mwendelezo wa kile ambacho watangulizi wake wamemtangulia.

Daima huwa kuna mambo makuu matatu kutoka serikali: Kuandaa sera na mitaala; kuwekeza kwenye miradi ya kielimu; pia inasimamia kuhakikisha inafanikiwa.

Hivi sasa kunashuhudiwa mabadiliko katika mfumo wa elimu shuleni. Mitaala, inafanyiwa mabadiliko makubwa, mfano kuanzishwa kwa tahasusi (combination) mpya katika kidato cha tano shuleni, ili kuendana na mahitaji ya sasa na ndio maana masomo ya lugha mpya kama za Kiarabu na Kichina zikiwamo, pia dhana ya kompyuta.

Pia, katika maboresho hayo, utawala wa nchi katika Awamu ya Sita umebadili mtaala kwenye mabadiliko makubwa yakionekana hasa kwa madarasa ya kwanza na pili, huku elimu ya msingi kuishia darasa la sita.

Hapo ikiangaliwa kisera, mabadiliko hayo yanachukua sura sasa anayeanza darasa la kwanza, anaendelea nayo hadi   kidato cha nne, tofauti na zamani kulikuwapo ‘kufaulu na kufeli.’

Kimsingi hilo sio geni, ikizingatiwa nchini Tanzania Bara iko katika awamu sita zote za chama kilekile, zinadumisha dhana ya ‘itikadi moja na kupokezana kijiti’, tofauti inayojitokeza ni maboresho kulingana na mahitaji ya wakati.

Hata dhana ya kisera ya kupanua wigo wa elimu ya sekondari kupitia uwekezaji wa kata, serikali ilianza nayo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi mnamo Julai mwaka 1988, ilipoanzishwa Shule ya Sekondari Kisarawe, ambayo sehemu kubwa iliwekezwa na wananchi wa Maneromango iliko shule.

Lakini wazo hilo likaboreshwa na Rais Benjamin Mkapa katika Awamu ya Tatu, akibuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).

Ni mkakati wa MMES uliosambza mno shule za sekondari kama ubunifu wa Maneromango, mwaka 1988, huku anayefuatia, Jakaya Kikwete katika Awamu ya Sita, akafanya maboresho makubwa ya alichoanzisha Mkapa.

Hapo nchini kukaneemeshwa ajira kwa walimu wengi kupunguza pengo la awali, kukitanuliwa ajira ya walimu iliyopunguza pengo la awali, walilotumia kutanua usaili wao katika vyuo vikuu nchini, hata kupata wahitimu wengi.

Hiyo haikushangaza, pale mwanamama Dk. Samia akapokea kijiti akiona pengo mojawapo akifanyia uwekezaji mkubwa.

Hilo ni la mabinti kuwatunulia wigo wa nafasi ya kuendelea kielimu, sasa nchini kuna mradi wa mabilioni kuwa na sekondari za mabweni mahsusi kwa wasichana, huku akiwakinga kisera hata wanaopata mimba, kuendelea na masomo.

Mzazi mara zote anaendelea kuwa sehemu ya nyenzo za mabadiliko tajwa, kwa kuwa ndio mfanikishaji mkubwa.

NAFASI YA WADAU 

Wadau katika elimu ni wengi kimsingi, kwa kuwa kila mtu ana mahitaji ya elimu, iwe rasmi au isiyo rasmi na ‘elimu haina mwisho.’

Elimu na wataalamu wa elimu huzalishwa na ndio maana haishangazi katika vyuo vikuu vyote duniani havikosi vitivo au shule za elimu.

Hao ndio wanakuwa katika sura moja wanaiangalia elimu nchini inavyoenda, wakishauri, kushirikiana nao, kuisifu na hata kuikosoa serikali inavyoendesha   elimu, lengo ni kusonga kuelekea kwenye ubora.

Huko nyuma, hata katika historia ya maboresho ya kuwa na sekondari ya kata nchini, inaanzia kwa walimu na Waziri mstaafu, akaishauri serikali akiwa nje ya Baraza la Mawaziri, ikapokewa kwa mafanikio ya MMES, ambayo leo shule hizo ndio nguzo za taifa.

Pia, wadau hao katika vyuo ngazi zote, ndio wanaonoa wataalamu hata kufanikisha mazao bora za kuzalisha wanafunzi bora shuleni. Mfano, Mzee Jackson Makweta, ni Waziri wa Elimu, pia Mkuu wa Shule nje ya Baraza la Mawaziri, ndiye aliibua wazo la kutanua sekondari za  kata katika awamu ya tatu.

ELIMU NI MTAJI

Hata inaporejewa historia ya nchi, hatua ya kwanza iliyofanywa na Mwalimu Nyerere katika miaka mitatu ya uhuru kukiwa hakuna sera ya muda mrefu, mwaka 1961 baada ya uhuru akatangaza elimu kwa wote shuleni, akiondoa mfumo wa kitabaka.

Pili, elimu nchini ikatengenezewa mwelekeo kisera, ikichukua sura tatu kuu; Elimu ya Shule Msingi, Elimu ya Vyuo na Elimu ya Watu Wazima.

Hata mwaka 1964, Mwalimu Nyerere katika Mpango wa wa miaka Mitano ya Uhuru 1964 – 1969, ukiwa ndio wa kwanza, uwekezaji mkubwa ulikuwa katika elimu ya msingi, lengo kutanua wigo kufikia wanafunzi wengi.

Ni dhamana hiyo ikafika mwaka 1976, serikali ikafika hatua tena serikali ikabeba dhamana yake kuandaa mtaala mpya wa elimu, ambao ukadumu muda mrefu, ukiendana na sera ilivyo, masomo kama elimu ya siasa. 

Ndio sasa, maboresho yanayoshuhudiwa kutanua wigo wa madarasa mahsusi kwa mabinti sekondari, huku mitaala ikiandaliwa mageuzi yaliyoanza kutumika Januari mwaka huu.