Bomba la mafuta lashusha neema ya maji jijini Tanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:27 PM Apr 16 2024
Kiongozi wa mbio za mwenge kwa mwaka huu, Godfrey Mnzava.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa mbio za mwenge kwa mwaka huu, Godfrey Mnzava.

ZAIDI ya wakazi 26,071 wa kata za Chongoleani, Mzizima na Mabokweni za Halmashauri ya Jiji la Tanga watapata maji kwa saa 24 kila siku baada ya kukamilika mradi unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA).

Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge kwa mwaka huu, Godfrey Mnzava wakati wa kuzindua mradi huo,  Mhandisi wa Miradi ya Maji Tanga UWASA, Violet Kazumba, alisema ulianza kujengwa Novemba mwaka 2022 na Mkandarasi wa jijini Dar es Salaam.

Kazumba alisema mradi huo umefadhiliwa na Taasisi  ya  ulazaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanzania.

Alisema usanifu wake unakadiriwa kugharimu kiasi cha Sh. 2,352,201,500 na hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh.1,823,766,540 sawa na asilimia 79.46.

Alisema mradi huo ulikamilika Machi mwaka huu kwa asilimia 100 na hadi sasa unatoa huduma kwa jamii na mamlaka hiyo inaendelea kuunganisha maji kwenye matawi na  watu binafsi.

Akizungumzia faida za mradi huo,  Kazumba, alisema utawezesha wakazi wa kata hizo kupata huduma ya maji safi kwa saa 24 kila siku.

Awali kiongozi wa mbio hizo za Mwenge, alisema ameridhishwa na utekelezaji mradi huo.
Mnzava alisema wamekuwa wakitekeleza maelekezo ya Serikali ya kutangaza miradi yote na zabuni kwenye Mfumo wa Kidigitali wa Zabuni (NEST).

Alisema wanaendelea kusisitiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa fedha kutoka serikali kuu, wahisani,wadau wa maendeleo na mchango wa wananchi.