Kigogo abanwa mwananchi kuuziwa bwawa, aamriwa kumrejeshea fedha

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 12:43 PM Apr 16 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita.

KAIMU Mwenyekiti wa Mtaa wa Shunu Kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Julius Sabuni ameamriwa kumrejeshea mwananchi Sh.550,000 baada ya kuuziwa eneo la bwawa la maji la Mtakuja kinyume na sheria.

Amri hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita   baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi  wakimtuhumu kigogo huyo kuuza eneo hilo bila ya kufuata taratibu .

Marco Masanja, mkazi wa eneo hilo, alisema aliuziwa sehemu ya bwawa hilo ili kujenga  makazi ya kudumu, lakini amezuiliwa kuendeleza ujenzi na wananchi kwa madai ni mali ya umma.

Alisema kabla ya kununua eneo hilo alifika katika Ofisi ya Mtaa wa Shunu na kukutana na Kaimu Mwenyekiti, Julius Sabuni kutaka kujua uhalali wa eneo hilo na kujibiwa kuwa halina tatizo na kununua kwa kiasi hicho.

"Mpaka sasa nimeshawekeza  Sh.milioni 1.2 ikiwemo kununua vifaa vya ujenzi, kusawazisha eneo, gharama za ununuzi. naomba nipewa fidia ya eneo lingine au kurejeshewa gharama zangu nilizotumia ili kuondoa malalamiko hayo kwani sio kosa langu na niliaminishwa na serikali kabla ya kununua,"  alilalamika Masanja.

Akijibu malalamiko hao, Sabuni alisema eneo hilo liliuzwa na mama mmoja ambaye kwa sasa yuko visiwani Zanzibar.

Alisema awali eneo hilo lilidaiwa kuwa ni mali ya umma, lakini mahakama ilitamka kuwa ni mali ya familia hiyo, hivyo hakuwa na shaka ya kushiriki kwenye mauziano hayo.

Alisema yukotayari kurejesha fedha  zilizotumika kununua eneo hilo na si Sh.milioni 1.2 kama inavyodaiwa na Masanja.

Sabuni alisema katika kikao walichokaa cha halmashauri ya maendeleo, walijadili na kumaliza mgogoro huo.

Akizungumzia mgogoro huo, Mboni alimtaka kaimu mwenyekiti huyo  kurejesha kiasi kilichotumika kununua eneo hilo kinyume na sheria na kuwasihi viongozi kutokuwa sehemu ya migogoro ya ardhi na badala yake wawe kwenye usuluhishi kwa kuwaeleza wananchi maeneo sahihi na ya umma.

Alisema kwa mujibu wa sheria za serikali za mitaa, wenyeviti hawaruhusiwi kusimamia mauziano ya ardhi na badala yake wanatakiwa kumtambulisha mnunuzi kwa mmiliki halali wa eneo.


Mkuu huyo wa wilaya alionya kuwa hatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wenyekiti wa serikali za mitaa watakaobainika kuhusika kwenye uuzaji wa maeneo ya umma na ya wazi kwani wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na kuichafua serikali.